Mkuu wa baraza la juu la usalama Iran aelekea Iraq, Lebanon
11 Agosti 2025Kiongozi wa Baraza la juu la Usalama la taifa la Iran Ali Larijani, anatarajiwa kuitembelea Iraq Jumatatu, kabla ya kuelekea Lebanon, ambako serikali imeidhinisha mpango wa kuwapokonya silaha wanamgambo wa Hezbollah ambao ni washirika wa Iran. Hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Larijani atatia saini makubaliano ya usalama ya pande mbili nchini Iraq kabla ya kuelekea Lebanon, ambako atakutana na maafisa waandamizi wa serikali ya Lebanon na viongozi wakuu.
Ziara yake Lebanon inafanyika baada ya Tehran kuonyesha upinzani mkali dhidi ya mpango wa serikali ya Lebanon kuwapokonya silaha Hezbollah, msimamo ambao Beirut ilikemea na kutaja kuwa "uingiliaji wa wazi na usikokubalika.”
Larijani amesema Iran inatambua "haki ya Lebanon kujilinda dhidi ya uchokozi wa utawala wa Israel akiongeza kuwa hilo "haliwezekani bila uwezo wa kijeshi na silaha.”
Kabla ya vita vyake na Israel, Hezbollah iliaminika kuwa na silaha nyingi zaidi kuliko jeshi la Lebanon.