Mkutano wa mwaka wa WHO umeanza mjini Geneva
19 Mei 2025Shirika la Afya Duniani (WHO) limefungua mkutano wake wa mwaka mjini Geneva leo Jumatatu kwa lengo la kupitisha rasmi mkataba wa kimataifa uliotarajiwa kwa muda mrefu kuhusu namna ya kupambana na kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza ambayo husababisha majanga duniani.
Mkataba huo ni matokeo ya athari za janga la Uviko-19 na unalenga kutengeneza mfumo sawa wa vifaa vya matibabu na kuhakikisha haki katika usambazaji wa chanjo kwa lengo la kuzuia majanga ya kiafya katika siku za usoni.
Mkutano huo wa WHO umewaleta pamoja wajumbe kutoka nchi wanachama 194.
Hata hivyo, WHO imo kwenye njia panda baada ya Marekani, ambayo ni mfadhili mkuu kutangaza kujiondoa mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2026, hatua ambayo itapunguza kwa kiasi kikubwa bajeti ya shirika hilo ambalo tayari limeshaanza kupunguza wafanyakazi wake na mipango ya misaada.