Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wafunguliwa Ethiopia
15 Februari 2025Mkutano huo umefunguliwa wakati juhudi za kidiplomasia zimeshindwa kuutatua mzozo wa Kongo ambapo waasi wa M23 wanaendelea kusonga mbele na jana wameukamata mji mwingine mkubwa wa Bukavu mashariki mwa nchi hiyo. Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema:
"Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, raia wa Kongo wanateseka kutokana na mzunguuko wa ghasia za kikatili. Na mapigano yanayoendelea huko Kivu Kusini kufuatia kusonga mbele kwa M23, yanatishia kulitumbukiza eneo lote kwenye janga. Ni lazima kuepusha kwa gharama yeyote, kuongezeka kwa mizozo ya kikanda. Hakuna suluhisho la kijeshi. Hali lazima isitishwe na mazungumzo yaanzishwe tena. Na uhuru na mipaka ya DRC ni lazima viheshimiwe."
Soma pia: Mzozo wa Kongo kutawala mkutano wa kilele wa AU
Mbali ya mizozo, mkutano wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa Halmashauri Kuu ya umoja huo atakayechukua nafasi ya Moussa Faki Mahamat anayemaliza muda wake. Wagombea watatu ikiwemo mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga wanawania nafasi hiyo.