Mkutano wa NATO waingia siku ya pili na ya mwisho
25 Juni 2025Mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana mjini The Hague Uholanzi, uliwakutanisha viongozi wa nchi wanachama wa NATO ambao walijadiliana kuhusu suala la kuongeza matumizi yao ya ulinzi, namna ya kuimarisha muungano huo pamoja na mizozo inayoendelea duniani ikiwa ni pamoja na ile ya Mashariki ya Kati na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alihutubia bunge la Uholanzi akituma pia ujumbe kwa viongozi wa NATO kuwa Urusi bado ni kitisho kwa kuwa imekuwa ikiunda ushirikiano na tawala za kikatili akisisitiza kuwa kutokana na msaada wa Iran, Moscow iliishambulia nchi yake kwa droni takriban 29,000 aina ya Shaheed, akisisitiza kuwa wasingelikuwa na uwezo wa kuzuia mashambulizi hayo bila ya msaada wa washirika wake wa Magharibi.
Uingereza kuimarisha jeshi lake kwa manufaa pia ya NATO
Uingereza kwa upande wake imerejelea kauli yake ya kuongeza pia matumizi yake ya ulinzi hadi kufikia asilimia 5 ya Pato la Taifa na kwamba itarejesha tena ndege za kivita chapa F-35A maarufu kama "Lockheed Martin" zenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia ili kutanua safu ya silaha ya nchi hiyo na kuimarisha jeshi la NATO . Kwa sasa Uingereza inayo makombora ya kurushwa kutoka chini ya bahari.
Katika taarifa, waziri Mkuu Keir Starmer amesema hatua hii ambayo ni ya kwanza tangu kumalizika kwa enzi za vita baridi inachukuliwa kwa kuzingatia nyakati za sasa zisizotabirika na zinazohitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya usalama hasa kutokana na kitisho cha Urusi na Marekani kuonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa Ulaya.
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte alipongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa mchango mwingine mkubwa wa Uingereza kwa jumuiya hiyo ya kijeshi, huku akisisitiza kuwa hana hofu juu ya utayari wa Marekani kuheshimu kifungu cha 5 cha mkataba wa jumuiya hiyo kuhusu dhamana ya usalama, ambacho kinaweka wazi kwamba nchi mwanachama anapovamiwa kijeshi, hatua hiyo huchukuliwa kama shambulio kwa wanachama wote wa NATO.
Trump akutana na Erdogan na kujadili mizozo inayoendelea
Pembezoni mwa mkutano huo, rais wa Marekani Donald Trump alikutana na mwenzake wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan na kujadili kuhusu mpango wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na Iran wakielezea matumaini yao kwamba mpango huo utakuwa wa kudumu.
Kwa pamoja, viongozi hao walitoa pia wito wa kufanyika mazungumzo ya kina katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine huku Erdogan akielezea wasiwasi wake kuhusu vita vinavyoendelea huko Gaza . Erdogan ametoa pia wito wa kuzidisha ushirikiano kati ya nchi yake na Marekani katika sekta ya ulinzi akisema kuwa inaweza kuimarisha kwa kiasi kikubwa biashara baina yao hadi kufikia lengo la kiasi cha dola bilioni 100. Mkutano huu wa NATO utaendelea na kumalizika leo Jumatano.
(Vyanzo: DPA, AFP, Reuters, AP)