Mkutano wa Kilele wa NATO waanza Uholanzi
25 Juni 2025Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema ana matumaini makubwa kwamba muungano huo wa kijeshi utakubaliana juu ya kuongeza matumizi katika mkutano huo wa siku mbili ambao ameuita kuwa wa mabadiliko. Viongozi wa nchi wanachama akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump wapo nchini Uholanzi.
Viongozi wa muungano huo wa mataifa 32 wanatarajiwa kukubaliana juu ya shabaha mpya ya matumizi ya ulinzi ya asilimia 5 ya Pato la Taifa, wakati ambapo Marekani ambayo ni mwanachama anayechangia fedha nyingi zaidi imeonesha kutotaka kuendelea na uchangiaji huo mkubwa kwa NATO na kuwakumbatia washirika wake wa Ulaya na badala yake imesisitiza kwamba inataka kuzingatia vipaumbele vya usalama mahala kwingine.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO, Mark Rutte, amesema ana imani kwamba muungano huo utakubali kuongeza matumizi ya ulinzi na kulifikia lengo la asilimia 5 licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wanachama.
Uhispania ni mojawapo ya nchi wanachama wa NATO iliyotangaza kuwa haitaweza kufikia lengo hilo la kuongeza fedha kwenye bajeti yake ya ulinzi kufikia tarehe mpya ya mwisho hapo mwaka 2035. Nchi nyingine ni Ubelgiji ambayo pia imeashiria kwamba haitaweza kulifikia lengo hilo huku Slovakia ikisema inataka kuitumia haki yake ya kuamua matumizi yake ya ulinzi.
Rais wa Marekani Donald Trump ameilaumu hatua ya Uhispania amesema ni dhuluma kwa wanachama wengine wa Jumuiyay a NATO.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, amethibitisha kwamba uamuzi wa washirika wa muungano wa NATO wa kuongeza matumizi ya ulinzi kwa kiasi kikubwa umechochewa na "kujiamini" kwa wanachama hao. Amesema wamefanya maamuzi hayo kulingana na mtazamo wao, imani yao na kwamba washirika wote wa NATO barani Ulaya ni lazima wachangie zaidi katika miaka ijayo ili kuweza kujisimamia kikamilifu katika swala la ulinzi.
Mkutano huo wa kilele wa siku mbili na wa kihistoria unaweza kuiunganisha Jumuiya ya kijeshi yenye wanachama 32 pale watakapokubaliana kwa kauli moja kupitisha ahadi mpya ya matumizi ya ulinzi au mkutano huo pia unaweza kuupanua mgawanyiko uliopo.