Mkutano wa BRICS mjini Rio waukosoa ushuru wa Trump
6 Julai 2025Mkutano wa kilele wa mataifa ya BRICS umehitimishwa kwa matamko makali dhidi ya sera za Marekani, wito wa kusitishwa kwa vita vya Gaza bila masharti, na kuungwa mkono kwa Iran kufuatia mashambulizi ya karibuni ya kijeshi kutoka Israel na Marekani.
Katika taarifa ya mwisho ya mkutano, viongozi wa BRICS — kundi la mataifa 11 yanayoinukia kiuchumi, yakiwemo Brazil, Urusi, India, China, Afrika Kusini, Iran na mengine — walieleza "wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hatua za ushuru wa upande mmoja na zisizo za ushuru ambazo zinapotosha biashara na hazilingani na kanuni za Shirika la Biashara Duniani (WTO)."
Tamko hilo lililenga moja kwa moja sera za Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amekuwa akiendesha vita vya kiushuru dhidi ya washirika na wapinzani wa kibiashara. BRICS ilizitaja hatua hizo kuwa haramu na za kiholela, na kuonya kwamba zinatishia kupunguza zaidi biashara ya kimataifa, kuathiri minyororo ya usambazaji, na kuleta hali ya sintofahamu katika shughuli za kiuchumi duniani.
Katika mwezi wa Aprili, Trump alitishia kutoza ushuru mzito kwa washirika wake wa kimataifa, kabla ya kupunguza kasi ya hatua hizo kutokana na kuyumba kwa masoko. Hata hivyo, ametoa onyo jipya kuwa makubaliano yasipofikiwa kabla ya Agosti 1, ushuru huo utarejeshwa.
Yataka kusitishwa mara moja kwa vita Gaza bila masharti
Kuhusu mgogoro wa Gaza, BRICS ilitoa wito wa dharura kwa pande husika kufikia usitishaji wa mapigano wa haraka, wa kudumu na usio na masharti yoyote.
Katika tamko lao, viongozi hao walihimiza mashauriano ya dhati baina ya Israel na Hamas, huku wakitaka kuondolewa kabisa kwa vikosi vya Israel kutoka Ukanda wa Gaza na maeneo mengine yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Tamko hilo limekuja wakati mazungumzo ya kusitisha vita yakiendelea mjini Doha. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, zaidi ya watu 57,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel — idadi inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa sahihi kwa ujumla.
Mkutano wa BRICS umejumuisha mataifa yenye msimamo mkali dhidi ya Israel kama Iran, pamoja na mataifa kama Urusi na China yenye uhusiano wa karibu na pande zote. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais Trump mjini Washington kujadili uwezekano wa makubaliano ya kusitisha vita.
Iran yapata ushindi wa kidiplomasia: Mashambulizi ya Marekani na Israel yalaaniwa
Katika hatua inayoonekana kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa Tehran, BRICS imelaani mashambulizi ya kijeshi yaliyolenga vituo vya kijeshi, nyuklia na miundombinu ya kiraia nchini Iran tangu tarehe 13 Juni 2025.
"Tunalaani mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," inasema taarifa ya mkutano huo. Ingawa Marekani na Israel hazikutajwa kwa majina, tamko hilo linaeleweka wazi kuwa linawalenga wao.
BRICS pia imeeleza "wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi ya makusudi dhidi ya miundombinu ya kiraia na maeneo ya nyuklia ya amani," ikiitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Iran ilikuwa imeshambuliwa kwa siku 12 mfululizo na Israel, ambapo baadaye Marekani ilitekeleza mashambulizi ya angani katika vituo vya nyuklia vya Natanz, Fordow na Isfahan.
Awali, wanadiplomasia wa BRICS walikuwa wamegawanyika kuhusu jinsi ya kulaani mashambulizi hayo, lakini baadaye walikubaliana kutumia lugha kali zaidi, kufuatia shinikizo kutoka Iran.
BRICS: Jukwaa la sauti ya kusini
Licha ya tofauti za ndani na changamoto za uongozi — hasa kutokuwepo kwa Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Urusi Vladimir Putin binafsi — mkutano wa mwaka huu umeonesha kuwa BRICS inataka kujidhihirisha kama sauti mbadala ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya mfumo wa dunia unaotawaliwa na mataifa ya Magharibi.
Kutoka katika onyo kwa sera za ushuru wa Marekani hadi msimamo kuhusu mizozo ya Mashariki ya Kati, BRICS inajitokeza kama jukwaa linalojaribu kuunda upya kanuni za uhusiano wa kimataifa.