mkutano mkuu wa kanisa katoliki nchini Ujerumani: 16-20.06.2004
17 Juni 2004Mkutano mkuu wa kanisa katoliki nchini Ujerumani uliofunguliwa rasmi Jumatano tarehe 16-Juni unafanyika kwa mara ya 95 mjini Ulm.
Kama kawaida ya mikutano hii ya kanisa, wageni kutoka kila upande nchini pamoja na nchi za nje hufika ili kushiriki kwenye mijadala mbalimbali ya kijamii na kidini.
Mwaka huu masuala ya utandawazi, kupanuka kwa Umoja wa Ulaya na kujongeana kwa madhehebu mabalimbali ni baadhi tu ya mada zilizopewa uzito wa juu kwenye hii siku maalumu ya Wakatoliki. Mada nyingine ni bima ya uzeeni na utata wa teknolojia mpya kama vile ya jeni kwa kufuatana na maadili.
Kiongozi wa jimbo la kanisa la Rottenburg-Stuttgart ambako mkutano wa kanisa katoliki mwaka huu unafanyikia, askofu Gerhard Fürst, alichambua wito wa kanisa katoliki mwaka huu, "kuishi kwa nguvu za Mungu" kwa kusema:"Kwenye kipindi hiki kilichotawaliwa na maendeleo ya kiteknolojia, watu wanaamini wanaweza kufanya kila kitu maishani, kama vile: ishi kwa nguvu zako mwenyewe. Lakini binadamu hujikuta kwenye hali ngumu anapotanabahi kwamba, uwezo wako una mipaka, na kwamba hawezi kuishi kwa nguvu zake mwenyewe."
Alisema askofu Fürst akiwakumbusha waumini na wageni wengineo kwenye mkutano huu maalumu kwenye siku ya wakatoliki wito wa "kuishi kwa nguvu za Mungu".
Mikutano hii ni muhimu sana na huwavutia watu wengi sana kwa makanisa yote makuu mawili nchini Ujerumani, kanisa katoliki na kanisa la kiinjili.
Zaidi ya ibada mbalimbali, mikutano hii hutumiwa kwa mijadala mbalimbali kuhusu maisha kwenye jamii. Matatizo ya ndani ya kanisa katoliki mwaka huu yanamulikwa pia – hususani madai ya mageuzi ndani ya kanisa hili. Kuna mapendekezo pia ya mambo nyeti kama vile kuondoa ulazima wa utawa kwa kuzingatia uhaba wa mapadri, kushirikishwa kwa wanawake kanisani na uhaba wa fedha.
Zaidi ya mambo haya kanisa katoliki (na mengine pia) linakabiliwa na lawama kwamba halijishughulishi vya kutosha na matatizo ya kijamii hivi sasa kama vile ukosefu wa kazi wakati mishahara ya mameneja inazidi kupanda. Tuhuma hizi zilitolewa hivi karibuni na aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha kihafidhina CDU, Heiner Geisler.
Hata hivyo kiongozi wa kanisa katoliki nchini, Hans Joachim Meyer, akipinga tuhuma hizi alisema, ugumu wa maisha kwa wananchi unatokana na makosa yaliyofanyika kwa muda mrefu kwenye sera za ustawi wa jamii. Kwa mantiki hii alisema, misingi ya sera hizi lazima ifanyiwe marekebisho ili serikali iendelee kuwasaidia watu hohehahe.
Kwa upande mwingine kanisa katoliki nalo linakabiliwa na upungufu wa waumini – kila mwaka wajerumani wengi wanajitoa kanisani, mara nyingi ili kukwepa kodi ya kanisa na wengine wanadai hawana muda, huku vijana wanadai kanisa halivutii. Hivi sasa Ujerumani kuna wakatoliki na waprotestanti milioni 53, lakini kila mwaka waumini 300,000 wanalipa mgongo kanisa. Aidha kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na jarida la FOCUS, siku hizi 1/7 ya wajerumani ndiyo huenda kanisani kila mara, na kwa wakatoliki peke yao ni mtu mmoja kati ya watu 10.
Lakini wahusika wanasema, umuhimu wa kanisa unaonekana wazi kwenye mikutano kama huu wa Ulm, ambapo maelfu ya watu wanahudhuria hafla mbalimbali. Baba mmoja amenukuliwa akisema mkutano huu ni muhimu sana kwa watoto:"Ni muhimu kuwaonyesha watoto picha nyingine ya kanisa – tofauti na ile tunayoiona kila siku kwenye kanisa letu."