Mkutano wa G7 kufunguliwa Canada katikati ya mizozo duniani
16 Juni 2025Mgogoro kati ya Israel na Iran, uliochochewa na mashambulizi ya kushtukiza ya kijeshi ya Israel na mashambulizi ya kisasi ya Iran, uliwashangaza viongozi wengi na mara moja ukatawala ajenda ya mkutano. Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais Trump wa Marekani, Donald Trump, wote wamefanya mazungumzo ya dharura na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakilenga kupunguza mivutano, ingawa hali bado ni ya wasiwasi mkubwa.
Katika taarifa iliyodhihirisha uzito wa mgogoro huo, afisa mmoja wa Marekani alithibitisha kuwa Rais Trump hivi karibuni alipinga mpango wa Israel wa kumuua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, jambo linaloonesha jinsi hali ilivyo karibu sana kuingia kwenye mwelekeo wa hatari zaidi. Wakati huo huo, Trump ameibua mjadala mwingine kwa kupendekeza Greenland iunganishwe na Marekani, na kutoa matamshi yaliyowakera wenyeji Canada.
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney alichagua kuvunja utaratibu wa kawaida kwa kutangaza kuwa hakutatolewa tamko la pamoja la mwisho, hatua inayolenga kuepuka kuonyesha migawanyiko mikubwa ndani ya G7, hasa kutokana na misimamo ya Trump isiyotabirika kuhusu biashara na diplomasia. Viongozi wa Ulaya wameamua kuzungumza naye moja kwa moja kwa lengo la kumshawishi asiweke ushuru mpya.
Vita vya Ukraine pia ni mada kuu ya mazungumzo hayo. Starmer alithibitisha kuwa vikwazo zaidi dhidi ya Urusi viko mezani endapo Rais Vladimir Putin ataendelea kupinga mapendekezo ya kusitisha mapigano. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo na kuomba msaada zaidi, baada ya kukubali mpango wa mazungumzo ya amani unaoungwa mkono na Marekani.
Changamoto lukuki kwa viongozi wa G7
Katika mazungumzo ya awali, Starmer na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni walisisitiza msaada wao kwa Kyiv na umuhimu wa kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu usalama. Starmer pia alidokeza kuwa ana mipango na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ya kuunda "muungano wa hiari” wa kutuma vikosi vya kulinda amani nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesisitiza hofu ya Ulaya juu ya kuyumba kwa masoko ya nishati kutokana na mgogoro wa Mashariki ya Kati. Akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano huo, von der Leyen alisema Umoja wa Ulaya na Marekani wanaendelea kushirikiana kwa karibu ili kutuliza masoko, ingawa hakufafanua hatua mahsusi zitakazochukuliwa kwa sasa.
"Basi mnapaswa kufahamu pia kuwa nimekubaliana na Rais Trump kwamba tunataka kupata suluhisho la pamoja kuhusu mazungumzo ya kibiashara kabla ya tarehe 9 Julai. Pia tunafanya kazi ya kupunguza vikwazo vya kibiashara", alisema Von der Leyen kabla ya kuongeza :
"Ndiyo maana tulitoa pendekezo la sifuri kwa sifuri - yaani, ushuru wa sifuri kwa bidhaa zote za viwandani pande zote mbili. Hili linapaswa kuwa ndilo lengo kwa muda mrefu. Lakini kwa sasa tuko katikati ya mazungumzo."
Kufika kwa Rais Trump nchini Canada kumeashiria mara ya kwanza kushiriki kwake kwenye mkutano wa G7 tangu arejee madarakani. Hata hivyo, uwepo wake unazua mjadala mkali, hasa kutokana na matamshi yake ya zamani ya kuitaka Canada kuwa "jimbo la 51 la Marekani” na sera zake za ushuru wa adhabu. Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, aliyechaguliwa kwa kampeni yenye msimamo mkali dhidi ya Trump, ameapa kutetea uhuru wa taifa lake na kuongoza mkutano wa kimaadili.