Mkataba wa UN Dhidi ya uchafuzi wa Plastiki Wakwama
14 Agosti 2025Wawakilishi kutoka nchi na mashirika 180 wamekuwa wakikongamana mjini Geneva Uswisi tangu Agosti 5, kusaka mkataba wa kimataifa utakaozuia uchafuzi plastiki ulimwenguni. Mazungumzo hayo yanayokamilika Alhamisi, yamedumu kwa muda wa wiki moja sasa lakini bado hakuna dalili ya kufikia makubaliano.
Hata hivyo washiriki hawakufutilia mbali uwezekano wa kurefusha mazungumzo hadi Ijumaa asubuhi.
Rasimu Yazua Hasira na Mgawanyiko Mkubwa
Katika juhudi za kujaribu kutafuta muafaka, mwenyekiti wa mazungumzo hayo Luis Vayas Valdivieso, aliwasilisha rasimu iliyojikita kwenye maeneo machache ya makubaliano.
Wanaharakati hata hivyo wataka kushawishi makubaliano hayo ya plastiki
Lakini rasimu hiyo ilitupiliwa mbali mara moja baada ya kuzusha ghadhabu miongoni mwa wajumbe wa pande zote. Mwakilishi wa Panama ambaye hakutambulishw jina amsema: "Rasimu iliyowasilishwa hapa yanawezesha kidonda kuua na hatukubali. Hii inachukiza tu. Ni kujisalimisha na hatutauza vizazi vyetu vijavyo kwa rasimu dhaifu kama hii.”
Kwa wanaoshinikiza mageuzi makubwa, rasimu hiyo ilikosa kuzingatia hatua madhubutizinazohitajika kama kudhibiti uzalishaji plastiki na kupiga marufuku viungo vyenye sumu kwenye uzalishaji. Badala yake, rasimu ikawa inazingatia jinsi ya kushughulikia taka za plastiki.
Mgawanyiko wa Kisiasa Watishia Mustakabali wa Dunia
Kwa upande wa nchi zenye mtizamo tofauti zinazoongozwa hasa na mataifa ya Ghuba, rasimu hiyo ilivuka mistari yao mingi nyekundu na haikutilia maanani matakwa yao.
Makubaliano hayo yanayosakwa ya Umoja wa Mataifa yanalenga kudhibiti uzalishaji, usanifu na usimamizi wa utupaji taka za plastiki.
Nchi zinazozalisha mafuta zinataka mazungumzo zilenge kuondoa taka za plastiki, lakini si kupunguza uzalishaji wa plastiki. Hii ni kwa sababu, kwa kiasi kikubwa bidhaa za mafuta ndizo hutumika kutengeneza plastiki.
Msimamo huo unakinzana na nchi nyingi hasa za Ulaya zinazosema kupunguza kwa taratibu uzalishaji wa plastiki ni moja ya masuala muhimu ya makubaliano.
Plastiki huchafua mazingira, huua Samaki na viumbe wengine . aidha huhatarisha maisha ya binadamu. Chembechembe za plastiki zinazidi kugunduliwa katika viungo vya binadamu ukiwemo ubongo.
Kulingana na tafiti, chembechembe hizo ndogondogo za plastiki huharibu mifumo ya kinga mwilini na huchochea maumivu.
(DPAE, AFPE,AFPTV)