Mkanganyiko kuhusu eneo la mkutano kati ya Marekani na Iran
15 Aprili 2025Mazungumzo muhimu kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran yanakabiliwa na sintofahamu juu ya mahali pa kufanyika, baada ya Iran kutangaza ghafla kuwa duru inayofuata ya mazungumzo itarejea tena Oman, licha ya viongozi kutoka Italia na Umoja wa Ulaya kusema kuwa mazungumzo hayo yangefanyika Rome wiki hii.
Marekani haijatoa tamko rasmi kuhusu mahali pa mazungumzo, lakini Rais Donald Trump amesema kasi ya mazungumzo hayo ni ya kusuasua na ametishia kuchukua hatua kali endapo hakutakuwa na maendeleo.
Mazungumzo haya yanafanyika wakati Iran ikiendelea kusafisha urani kwa kiwango cha hadi asilimia 60, hatua ambayo iko karibu na kiwango cha kutengeneza silaha za nyuklia.
Soma pia:Iran na Marekani zajiandaa kukutana tena wiki hii kujadili Nyuklia ya Iran
Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi, anatarajiwa kuwasili Tehran kuzungumzia upatikanaji wa taarifa zaidi kwa wakaguzi wake kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Mpango wa awali wa mwaka 2015 uliiweka Iran chini ya masharti ya kupunguza kiwango cha urani, na kwa kubadilishana ilipatiwa unafuu wa vikwazo.
Tangu Marekani ijiondoe katika makubaliano hayo mwaka 2018, Iran imeongeza shughuli zake za nyuklia huku ikisisitiza kuwa haitakubali mashinikizo ya kisiasa bila dhamana madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano mapya.