Mjumbe wa Trump akutana na wawakilishi wa DRC na Rwanda Doha
30 Aprili 2025Mkutano huo umetokea baada ya pande hizo mbili – Kongo na Rwanda - kukubaliana kuanza mazungumzo ya kumaliza mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Boulous, mfanyibiashara ambaye pia ni mkwe wa Rais wa Marekani, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, alikutana pia na maafisa kutoka Ufaransa, Qatar na Togo, ambayo ni mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro huo.
Amesema mkutano huo unapania kuendeleza "dhamira ya pamoja ya kuleta amani, utulivu na ustawi katika kanda ya maziwa makuu."
Soma pia: DR Kongo, M23 watoa ahadi ya pamoja kufikia mapatano
Wizara ya mambo ya nje ya Qatar imeeleza katika taarifa kuwa, mazungumzo hayo yalijikita kwenye mgogoro wa Kongo, majadiliano yanayoendelea kati ya pande zinazohasimiana na hali ya kibinadamu ambayo inahitaji mwitikio wa haraka na wa pamoja.
Nchi hiyo ya Ghuba imekuwa mpatanishi katika mgogoro wa Kongo ulioibuka tena katika miezi ya hivi karibuni.