Mjumbe wa Trump akutana na Putin kujadili vita vya Ukraine
25 Aprili 2025Mjumbe wa Marekani Steve Witkoff amewasilisiku ya Ijumaa mjini Moscow na kukutana kwa mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin na kujadili namna ya kuumaliza mzozo huo.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema bado kuna vipengele kadhaa vya makubaliano na Marekani kuhusu kumaliza vita nchini Ukraine, ambavyo bado vinahitaji kurekebishwa huku akiamini kuwa mchakato huo upo kwenye mwelekeo sahihi.
Soma pia: Ukraine yasema haitatambua uhalali wa Urusi kuidhibiti rasi ya Crimea
Wakati huohuo, Meya wa jiji la Kiev Vitali Klitschko amesema Rais Volodymyr Zelenskiy huenda akatakiwa kukubali suluhusho la kufikia amani, ambalo litamlazimu kukubali kuyaachia maeneo yaliyonyakuliwa na urusi, licha ya kuwa watu wa Ukraine kamwe hawatokubali ardhi yao kukaliwa na Urusi.
Matamshi ya Klitschko yametolewa wakati rais wa Marekani Donald Trump amesema katika mahojiano na gazeti la TIME kwamba eneo muhimu la Rasi ya crimea lililonyakuliwa na Urusi mwaka 2014 na ambalo limekuwa kiini cha mzozo kati ya Moscow na Kiev litasalia kuwa chini ya udhibiti wa Urusi na kwamba rais Volodymyr Zelensky analielewa hilo. Hata hivyo Marekani haikutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo wa amani unaojadiliwa kuhusu mzozo huo kati ya Urusi na Ukraine.
Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana vikali
Watu watano wameuawa sehemu mbalimbali nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na watatu katika mji wa Pavlohrad huko Dnipropetrovsk kufuatia mashambulizi ya Urusi. Watu wengine karibu 14 wamejeruhiwa. Usiku wa kuamkia Ijumaa, na watu wengine 12 wameripotiwa kuuawa mjini Kiev.
Soma pia: Trump atoa wito kwa Urusi kusitisha mashambulizi Ukraine
Pia, gari iliyokuwa na vilipuzi imeripuka mjini Moscow leo Ijumaa na kusababisha kifo cha afisa mwandamizi wa jeshi la Urusi ambaye alitambuliwa kuwa ni Luteni Jenerali Yaroslav Moskalik, aliyekuwa naibu mkuu wa kamandi kuu anayehusika na masuala ya operesheni za jeshi. Svetlana Petrenko, msemaji wa Kamati ya Uchunguzi ya Urusi amesema:
"Timu ya uchunguzi inayojumuisha wachunguzi, wataalam wa kitabibu na maabara pamoja na maafisa wa sheria imeanza kulifanyia uchunguzi wa kina eneo la tukio."
Serikali ya Ukraine haijazungumzia chochote kuhusu shambulio hilo, ambalo linashabihiana mno na mfumo wa mauaji iliyoyafanya dhidi ya maafisa wa kijeshi wa Urusi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
(Vyanzo: Mashirika)