Kellog aitaka Urusi isitishe vita Ukraine
14 Julai 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye muda mfupi uliopita amemteuwa Yulia Svyrydenko kuwa waziri mkuu mpya, amesema mazungumzo yake ya mjumbe wa Marekani Keith Kellog anayeitembelea Kiev, yamekwenda vizuri.
Zelenskyamesema amejadili pamoja na mjumbe huyo maalum wa Marekani, kuhusu ulinzi wa anga, silaha pamoja na suala la vikwazo dhidi ya Urusi.
''Tunamshukuru rais Trump kwa ujumbe wake na maamuzi mazito aliyoyafanya kuhusu kuanza kutuletea tena silaha.Na tunashukuru uungaji mkono wa vyama vyote Marekani. Na bila shaka tulikuwa na mazungzumzo mazuri na Trump huko The Hague na kwenye simu.Tumefanya maamuzi kadhaa chanya kwa nchi zote mbili na hivi punde tumejadili kuhusu ulinzi wa anga na jenerali Keith Kellogg.
Kellog ambaye aliwasili mapema leo mjini Kiev, ameitolea mwito Urusi isitishe vita mara moja na kuingia kwenye mazungumzo ya pande tatu, akisema nchi hiyo haiwezi kuendelea kuvuta muda huku ikiendelea kushambulia maeneo ya makaazi nchini Ukraine.