Mjumbe maalum Steve Witkoff atembelea kusini mwa Gaza
1 Agosti 2025Mjumbe maalum Steve Witkoff na Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee, wametembelea eneo moja kati ya maeneo manne yaliyo na vituo vya usambazaji vinavyoendeshwa na Taasisi ya Misaada ya GHF katika mji wa kusini wa Rafah.
Maeneo yote manne ya usambazaji yapo katika kanda zinazodhibitiwa na jeshi la Israel tangu lilipoanza operesheni yake Gaza.
Ziara ya mjumbe maalum wa Rais Donald Trump katika eneo la Mashariki ya Kati, pia inaenda sambamba na ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, ambalo limeyalaumu majeshi ya Israel kwa kuchukulia kuwa ni jambo la kawaida kumwagika damu katika vituo vya GHF, taasisi ya misaada inayoungwa mkono na Marekani. Taasisi hiyo imekuwa inakosolewa tangu kuanzishwa kwake mwishoni mwa mwezi Mei.
Ofisi ya haki ya Umoja wa Mataifa katika ardhi ya Palestina imesema takriban watu 1,373 wameuawa wakitafuta msaada huko Gaza tangu Mei 27, 105 kati yao wameuawa katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
Katika ripoti yake kuhusu vituo vya GHF, Shirika la Human Rights Watch ilimelilaumu jeshi la Israel kwa kuvunja sheria na kuitumia njaa kama silaha ya vita.
Likijibu ripoti hiyo, jeshi la Israel limesema taasisi ya GHF inafanya kazi kwa uhuru, na kwamba wanajeshi wa Israel wanafanya kazi karibu na maeneo mapya ya usambazaji ili kuwezesha utoaji wa chakula kwa utaratibu mzuri. Jeshi la Israel limelilaumu kundi la Hamas kwa kuzuia usambazaji wa chakula na limesema linafanya mapitio ya vifo vilivyoorodheshwa, na kwamba linaongeza juhudi iwezekanavyo kupunguza, misuguano kati ya raia na vikosi vyake.
Wakati huo huo waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ameionya Israel kutokana na msimamo wake wa kutaka kuutwaa Ukingo wa Magharibi.
Wadephul wakati wa ziara yake katika eneo la Palestina siku ya Ijumaa pia amelaani vikali juu ya kuongezeka kwa ghasia za walowezi wa Kiyahudi dhidi ya wakazi wa Palestina.
Baada ya mkutano wake na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah, Waziri huyo wa mambo ya Nje wa Ujerumani amesema nchi yake inaunga mkono haki ya Wapalestina kuwa na nchi yao wenyewe baada ya kukamilika mchakato wa kisiasa. Amesema Ujerumani pia iko tayari kuunga mkono kikamilifu mchakato wa ujenzi mpya baada ya kumalizika vita katika Ukanda wa Gaza.
Nchi kadhaa zimeanza juhudi za kudondosha misaada kwa watu wa Palestina. Ujerumani imejiunga kwenye juhudi za kimataifa za kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu katika eneo la Palestina lililozingirwa.
Wizara ya Ulinzi ya Ujerumani imesema ndege za jeshi la Ujerumani siku ya Ijumaa zimedondosha vifurushi 34 ambavyo kwa ujumla wake ni takriban tani 14 za chakula na vifaa vya matibabu katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema nchi yake inashiriki katika operesheni hiyo ikiwa na ndege mbili, zinazopakiwa katika kituo cha kijeshi huko nchini Jordan. Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania na Uingereza zimeungana na msururu wa mataifa mengine ya Magharibi kupeleka misaada Gaza kwa njia ya kuidodonsha kutoka angani huku hofu ya kuzuka baa la njaa ikiongezeka katika eneo hilo.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba Gaza iko ukingoni kutumbukia kwenye baa la njaa. Mashirika ya misaada yamekosoa juhudi za kudondosha misaada kutoka angani yamesema hazikidhi mahitaji makubwa ardhini.
Philippe Lazzarini, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina amesema shughuli ya kudondosha misaada kutoka hewani ni ghali mara 100 kuliko kufikisha misaada hiyo kwa njia ya ardhini kwa sababu malori yanaweza kubeba misaada mara mbili zaidi ya ndege.
Vyanzo: RTRE/DPA/AP/AFP