RSF yaushambulia mji wa Port Sudan kwa droni
5 Mei 2025Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, vikosi vya RSF viliilenga Kambi ya Anga ya Osman Digna, ghala la bidhaa, pamoja na miundombinu ya kiraia kwa kutumia angalau ndege saba zisizo na rubani.
Kamanda wa Kanda ya Kijeshi kwenye Bahari ya Shamu amesema mashambulizi hayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu na yalihusisha jumla ya droni 11. Hakuna vifo vilivyoripotiwa, ingawa uharibifu wa mali umetokea.
Shambulio hilo liliibua hofu na kusababisha uwanja wa ndege wa Port Sudan kusitisha shughuli kwa muda na mamlaka ya usafiri wa anga. Uwanja huo umekuwa kiunganishi muhimu tangu uwanja wa ndege wa Khartoum ulipofungwa mwanzoni mwa vita.
Wakati huo huo, RSF iliushambulia pia Uwanja wa Ndege wa Kassala ulioko karibu na mpaka wa Eritrea, siku moja tu baada ya shambulio la awali.
Katika mji wa El-Obeid, wakazi waliripoti kuona droni zikizunguka angani kabla ya milipuko kusikika. Hili linaonyesha matumizi ya droni kuwa silaha mpya ya RSF kupanua vita mbali na ngome zao.
Soma pia:Kambi ya jeshi la anga la Sudan yashambuliwa kwa droni
Maafisa wa Sudan wameushutumu Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa kutoa droni za kisasa kwa RSF. Waziri wa Habari wa Sudan, Khalid al-Eisir, amesema mashambulizi hayo yalipangwa na kuendeshwa kutoka Abu Dhabi, jambo linalowafanya wavione vita hivyo ni tishio la kimataifa na si la ndani pekee. Umoja wa Falme za Kiarabu umekana madai haya mara kadhaa.
Kulipiza kisasi, jeshi la Sudan lilishambulia Uwanja wa Ndege wa Nyala katika jimbo la Darfur na kudai kuharibu ndege ya mizigo aina ya Boeing kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu iliyokuwa ikibeba silaha, droni na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya RSF.
Jeshi limesema raia wa kigeni na wapiganaji 150 wa RSF waliokuwa wakipelekwa Imarati kwa mafunzo ya kijeshi waliuawa kwenye shambulio hilo.
Wachambuzi: Mashambulizi yanalenga kuleta hofu
Mgogoro huu uliibuka kutoka kwenye mvutano wa madaraka kati ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa jeshi la serikali na kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo.
Baada ya kupoteza udhibiti wa Khartoum, RSF wamejikita zaidi katika mikoa ya Darfur na maeneo ya kusini, huku jeshi likidhibiti maeneo ya kati, mashariki na kaskazini mwa nchi.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kampeni ya mashambulizi ya RSF kwa kutumia droni inalenga kusababisha hofu, kuvuruga usambazaji wa vifaa vya kijeshi, na kupunguza nguvu ya jeshi katika maeneo linaloyadhibiti. Bila kurejesha maeneo waliyoyapoteza, RSF wanaonekana kutegemea zaidi mashambulizi ya angani.
Soma pia:Takriban watu 542 wameuwawa Sudan ndani ya wiki tatu
Mashirika ya haki za binadamu na Umoja wa Mataifa yamewashutumu hasa RSF kwa uhalifu mkubwa wa kivita, ikiwemo mauaji ya kikabila, ubakaji wa halaiki, na mashambulizi dhidi ya raia, hasa katika maeneo ya Darfur. Matukio haya yanachunguzwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Tangu vita vianze Aprili 2023, takriban watu 24,000 wameuawa na milioni 13 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, wakiwemo milioni 4 waliokimbilia nchi jirani. Mgogoro huu umevuruga kabisa miundombinu ya Sudan, kuharibu maisha ya mamilioni na kusababisha njaa katika sehemu kadhaa za nchi.