Nagasaki yaadhimisha miaka 80 tangu kushambuliwa na Marekani
9 Agosti 2025Kengele mbili za kanisa kuu katika mji huo zililia kwa pamoja na kwa mara ya kwanza tangu shambulio hilo ili kuadhimisha tukio hilo la kutisha. Takriban watu 2,600, wakiwemo wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 90 wamehudhuria maadhimisho hayo katika eneo linalofahamika kama "Hifadhi ya Amani ya Nagasaki", ambapo Meya wa mji huo, Waziri Mkuu Shigeru Ishiba na viongozi wengine walihutubia.
Katika hotuba yake, Meya wa Nagasaki Shiro Suzuki ameutolewa wito ulimwengu kukomesha mara moja migogoro ya silaha huku manusura wakitahadharisha kuhusu matumizi ya silaha za atomiki hasa katika migogoro ya sasa.
Mnamo Agosti 9 mwaka 1945, majira ya saa tano na dakika mbili asubuhi, siku tatu baada ya shambulio la nyuklia huko Hiroshima lililosababisha vifo vya watu 140,000, Marekani iliangusha bomu la atomiki huko Nagasaki na kuwauawa watu zaidi ya 70,000. Matokeo yake, Japan ilisalimu amri tarehe 15 mwezi Agosti na kuhitimisha Vita vya Pili vya Dunia na uvamizi wake wa nusu karne barani Asia.