Mjadala katika Bunge la Ujerumani kuhusu mzozo ndani ya Jumuiya ya Ulaya
16 Juni 2005.
Baada ya katiba ya Ulaya kukataliwa na wapiga kura wa Ufaransa na wa Uholanzi, sasa Jumuiya ya Ulaya iko katika mzozo. Hayo yalisemwa na Kansela Schroader. Hata hivyo, alisema zoezi la kuipa kibali katiba hiyo bora liendelezwe katika nchi nyingine wanachama wa Jumuiya.
Insert: O-Ton Schroader:
+Nchi kumi zimeukubali mkataba huo wa katiba ya Ulaya, nyingine zimetangaza zitaukubali mkataba huo. Sasa mtu anasikia maneno kutoka bunge la Ulaya kwamba katiba hiyo imekufa au kitu kama hicho. Hivyo sivyo kabisa na matamshi hayo yanadharau namna vile sisi tulivoamua.+
Kansela Schroader alipendekeza kwamba mwanzoni mwa mwakani inafaa baraza la viongozi wa nchi za Jumuiya likae lizingatie, na licha ya matatizo yaliotokea mwenedo wa kuipanua Jumuiya lazima uendelezwe, kwa vile kurejea katika uzalendo wa zamani sio njia mbadala. Kansela alitaka Romania na Bulgaria ziingizwe katika Jumuiya na yaanzishwe mashauriano yenye madhumuni ya kuiingiza pia Uturuki.
Insert: O-Ton Schrader:
+ Namuonya kila mtu ambaye anafikiri anaweza kuyatupilia mbali majukumu yaliokubaliwa, au angalau kuyaweka pembeni. Ninaonya.+
Bibi Angela Merkel, mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya vyama vya CDU/CSU, alionya juu ya kuipanua bila ya mipaka Jumuiya ya Ulaya. Alisema chama chake kitaipa Uturuki nafasi ya ushirika wa upendeleo, lakini sio uwanachama wa Jumuiya. Kwa mujibu wa mtizamo wa Bibi Merkel ni kwamba kura za Wafaransa na Waholanzi za kuikataa katiba ya Ulaya zimedhihirisha kwamba Jumuiya haitilii manani hofu za raia.
Insert: O-Ton…
+ Kwanza: nasema tuachane na kuivuta sana ndani Ulaya . Kwa watu wengi, wao wanaiona Jumuiya ya Ulaya kama urasimu mkubwa, watu hao hawaifahamu jumuiya hiyo na hawawezi kuiona; na kwamba Jumuiya kwa kweli inajihusisha tu na masuala ya Ulaya.+
Bibi Merkel alisema kutoka mkutano wa kilele wa nchi za Jumuiya unaoanza leo lazima kutolewe ishara kwamba mambo hayawezi kwenda kama yalivokuwa hapo kabla, ama sivyo Ulaya itavurugika.
Uwezo wa kuvurugika Ulaya kwa sasa umeonekana katika mzozo uliochipuka kuhusu bajeti ya jumuiya. Kansela Schroader amesema Ujerumani haimudu kuengeza sana mchango wake katika bajeti ya Jumuiya, lakini iko tayari kufikia suluhu. Lakini pia Uengereza inatakiwa iwe tayari kufikia suluhu. Ile afuweni na nafuu ambayo Uengereza imekuwa ikiipata kwa zaidi ya miaka 20 iliopita katika michango yake ya fedha ndani ya Jumuiya haistahili na sio ya haki. Kansela Schroader, hata hivyo, aliyaweka chini matumaini kwamba katika mkutano wa sasa wa kilele wa Jumuiya kunaweza kukapatikana muwafaka katika masuala haya ya mabishano.
Miraji Othman