Misri na Qatar zawasilisha pendekezo jipya kwa Hamas
15 Aprili 2025Hamas imesema katika taarifa yake kwamba makubaliano yoyote yatapaswa kujumuisha hatua ya kudumu ya kusimamisha vita na kuondoka kwa wanajeshi wote wa israeli kwenye Ukanda wa Gaza.
Aidha wapalestina wanataka mpango wa dhati wa kubadilishana wafungwa, njia makini ya kuelekea kwenye ujenzi mpya na kuondolewa vizuizi kwenye Ukanda wa Gaza. Hapo awali kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kiliripoti kwamba wapiganaji wa Hamas wamelikataa pendekezo la Israel la kutaka wapiganaji hao wapokonywe kabisa silaha kama sharti la kusimamisha mapigano.
Wajumbe wa Israel na wapalestina kwa sasa wanafanya mazungumzo, ambayo si ya ana kwa ana juu ya kufikia makubaliano mapya ya kusimamisha mapigano baada ya juhudi za hapo awali za kurefusha hatua ya kusimamisha mapigano kushindikana.
Israel ilianzisha tena mashambulio kwenye Ukanda wa Gaza hivi karibuni na kuwatupia lawama Hamas juu ya kukwama kwa mazungumzo.