Mipango ya siri ya kijeshi ya Marekani yavuja
25 Machi 2025Mhariri Mkuu wa jarida la The Atlantic, Jeffrey Goldberg, alisema Jumatatu kwamba alijumuishwa kwa bahati mbaya katika mazungumzo ya siri ya serikali ya Marekani yaliyofanyika kupitia mtandao wa kijamii wa Signal, ambayo yalijadili mipango muhimu na ya siri ya kijeshi kuhusu shambulizi dhidi ya wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, nchini Yemen.
Maafisa waliohusika katika mazungumzo
Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo ya kikundi hicho yaliyofanyika kupitia mtandao wa mawasiliano wa Signal, yaliwahusisha maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Rais Trump, akiwemo Makamu wa Rais JD Vance, Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
Katika taarifa iliyochapishwa Jumatatu, Goldberg alielezea jinsi alivyojumuishwa kwa bahati mbaya kwenye mazungumzo hayo katikati ya mwezi Machi. Awali alisema hakudhani kama ni ya kweli.
Kulingana na Goldberg, alikuwa na mashaka makubwa kama mazungumzo hayo yalikuwa ya kweli, kwa sababu hakuamini kwamba maafisa wa usalama wa taifa wa Marekani wanaweza kuwasiliana kupitia mtandao huo wa Signal kuhusu mipango ya vita.
Brian Hughes, msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa, amethibitisha kwamba historia ya mazungumzo ilionekana kuwa ya kweli na ametangaza kufanyika uchaguzi wa ndani kuhusu tukio hilo.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth amesema hakuna mtu aliyekuwa anatuma ujumbe kuhusu mipango ya vita katika mazungumzo ya kikundi hicho. Pia alizungumzia kuhusu kuingizwa kwa makosa mwadishi huyo wa habari.
Trump asema hana taarifa
''Unamzungumza kuhusu mtu anayeitwa mwandishi habari mdanganyifu na aliyedharauliwa sana? Nimesikia hivyo. Hakuna mtu aliyekuwa anatuma ujumbe kuhusu mipango ya vita. Na hayo ndiyo yote ninayopaswa kusema kusema kuhusu hilo. Asante. Ni hivyo tu,'' alisisitiza Hegseth.
Alipoulizwa kuhusu kuvuja kwa mazungumzo hayo, Rais Trump alisema hajui lolote kuhusu hilo. Hata hivyo, baadae Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House, Karoline Leavitt alisema Rais Trump anaendelea kuwa na imani kubwa na timu yake ya usalama, akiwemo Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, ambaye inasemekana ndiye alimjumuisha Goldberg kwenye mazungumzo hayo.
Tukio hilo limezusha mkanganyiko, huku viongozi wa upinzani katika Baraza la Seneti la Marekani wakitoa wito wa kufanyika uchunguzi kamili.
Chuck Schumer, kutoka chama cha Democratic ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika Baraza la Seneti amelielezea tukio hilo kama uvunjaji wa utolewaji wa taarifa za siri na jinsi watu wanavyouawa.
Schumer ameelezea katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X jinsi maadui wao watakavyofaidika nalo, na jinsi usalama wa taifa la Marekani unavyoingia hatarini.
(DPA, DW)