Mioto inavyoangamiza misitu Kenya – Nani wa kulaumiwa?
28 Aprili 2025"Joto linapopanda, miti hukauka, nyasi pia, moto kidogo tu umetosha kuwakisha msitu mzima.” Kauli hii inaakisi hali halisi ya Kenya ambapo mabadiliko ya tabianchi na ukame vimezidisha hatari ya moto misituni. Katika kipindi cha Januari hadi Februari pekee, zaidi ya maeneo 180 ya misitu na hifadhi za wanyama yaliripotiwa kuteketea kwa moto.
Visa vingi viliripotiwa katika Msitu wa Kajulu (Kisumu), Msitu wa Nandi (Bonde la Ufa), na Mbuga ya Ruma (Homa Bay). Moto huu mara nyingi huzushwa na shughuli za kibinadamu kama kuchoma taka, kuandaa mashamba au kuvuna asali kwa kutumia moto.
Mkazi wa Kakamega, Daudi Oduor, anasema: "Watu huwashia moto mashambani lakini hauwezi kudhibitiwa. Mwisho wake huathiri misitu jirani.”
Athari kwa viumbe hai na maisha ya watu
Mbali na kuharibu miti, moto huu unaathiri maisha ya viumbe hai na wanadamu. Misitu inayoteketea ni makazi ya ndege wanaohama kutoka Ulaya na Amerika, na ni vyanzo vya maji kwa jamii. Benedict Adero, mwanaharakati wa mazingira, anaeleza kuwa asilimia 70 ya msitu wa Kajulu tayari imeungua, huku chemichemi ya Dunga katika Ziwa Victoria ikihatarishwa pia.
Soma zaidi: Moto wa nyika
Pamoja na hayo, jamii zinazotegemea misitu kwa ajili ya ufugaji wa nyuki, utalii wa ndege na uvunaji wa mbao kwa mujibu wa sheria hupoteza vipato. Kwao, moto huu si tu janga la mazingira bali pia ni la kiuchumi.
Kwa mujibu wa KFS, zaidi ya hekta 1,500 za misitu zimepotea kutokana na mchanganyiko wa ukame, upepo mkali na shughuli za kibinadamu.
Njia ya kukabiliana na janga hili
Changamoto kubwa ni ukosefu wa vifaa na mafunzo kwa jamii zinazohitajika kusaidia kuzima moto. Chrispine Osunga kutoka Homabay analalamikia ukosefu wa elimu na bima kwa raia wanaojitolea kusaidia. "Wanapoitwa kusaidia, hawajui la kufanya na hata wakijeruhiwa, hawana bima kama askari,” anasema.
Hata hivyo, kuna matumaini. Ushirikiano mzuri kati ya serikali na jamii umeonesha mafanikio katika maeneo kama msitu wa Old Bonjoge na Kobujoi, ambako wakazi wanaruhusiwa kulima huku wakihitajika pia kutunza miti.
Serikali inalenga kupanda miti bilioni 15 kufikia 2032 ili kuongeza maeneo ya miti hadi asilimia 30 ya nchi. Aidha, teknolojia mpya za kutambua moto mapema zinaendelezwa, na sheria mpya zimewekwa kuwazuia watu kuchoma mimea karibu na misitu bila kibali.
Moto unaoteketeza misitu si tu tatizo la asili—ni changamoto ya kijamii, kiuchumi na kiusalama. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuilinda misitu kwa kupanda miti, kuelimisha jamii, na kushiriki katika juhudi za pamoja za kuhifadhi mazingira. Mazingira ni maisha—tuyatunze!