Milipuko yautikisa mji wa Port Sudan
7 Mei 2025Milipuko ilisikika katika mji huo, ingawa haikuwa wazi wakati huo iwapo ilifanyika karibu na kambi ya Flamingo.
Mji wa Port Sudan umekuwa ukishambuliwa kwa siku kadhaa sasa - yakiwemo mashambulizi yanayoripotiwa kufanywa na wanamgambo wa RSF - ambao waliziteketeza hifadhi kubwa za mafuta nchini humo na kuharibu njia ya pekee ya kuingiza misaada ya kiutu.
Mji huo ulio katika Bahari ya Sham kwa sehemu kubwa ulikuwa haujafikiwa na mapigano tangu kuanza kwa vita hivyo kati ya jeshi la wanamgambo wa RSF mnamo Aprili 2023. Vita hivyo vilisababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makaazi yao, ukosefu mkubwa wa chakula na mauaji yaliyochochewa kikabila.
Mji wa Port Sudan ulikuwa makao ya serikali inayojitanabahisha na jeshi la nchi hiyo baada ya wanamgambo wa RSF kuchukua sehemu kubwa ya Mji Mkuu Khartoum mwanzoni mwa vita hivyo.
Mashambulizi ya hayo ya droni yamefungua eneo jipya la mapigano baada ya jeshi hivi majuzi kuchukua udhibiti katika mji mkuu na Sudan ya kati.
Vita vya Sudan vilizuka kufuatia mivutano ya mamlaka kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF na kutokea wakati huo, pande zote mbili zimepata uungwaji mkono kutoka kwa marafiki zake wa kigeni.
Vyanzo: Reuters/AFP