Miito ya haki yahanikiza mchuuzi aliyepigwa risasi Kenya
19 Juni 2025Boniface Kariuki, baba mzazi wa Johan amewaambia waandishi habari kuwa mtoto wake huyo wa pekee anapigania maisha kwenye wodi ya wagonjwa mahututi baada ya kupigwa risasi ya kichwa. Amesema alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa wa kuondoa risasi Jumanne usiku.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 na mchuuzi wa bidhaa ndogondogo inaaminika alijipata katikati ya mapambano na polisi wawili waliokuwa wakipambana na maandamano ya vijana yaliyofanyika mjini Nairobi kulaani mauaji ya mwanablogu aliyekuwa rumande.
Polisi mmoja aliyefunika uso alimpiga risasi ya kichwa Jonah na kuondoka. Jeshi la polisi limesema limewakamata maafisa hao wawili na wanahojiwa.
Kisa hicho kimezidisha hasira na mashaka kuhusiana na madai ya kila wakati ya ukatili wa polisi kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.