Israel yabadili idadi ya vifo vya shambulizi la Oktoba 7
11 Novemba 2023Kulingana na jeshi la Israel zaidi ya wakaazi 100,000 kwenye Ukanda wa Gaza wamekimbilia kusini mwa eneo hilo katika kipindi cha siku mbili zilizopita wakati vikosi vyake vikizidi kushambulia katikati mwa mji wa Gaza.
Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema wakati akiarifu juu ya mzozo huo kwamba juhudi za kuhakikisha mateka wanaachiwa zinaendelea, ingawa amesisitiza kwamba juhudi kama hizo huwa zinachukua muda mrefu.
Karibu watu 240 walichukuliwa mateka katika shambulizi la wanamgambo wa Hamas waliovamia jamii zilizokuwa zinaishi kusini mwa Israel, mnamo Oktoba 7. Israel pia imebadili idadi ya vifo vilivyotokea kwenye shambulizi hilo kutoka watu 1,400 hadi 1,200. Hayo yameelezwa na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo Lior Haiat alipozungumza na shirika la habari la AFP.
Amesema idadi hiyo ya vifo 1,200 ndiyo halisi na ile iliyotolewa awali ilijumuisha wanamgambo wa Hamas waliouwawa ambao wamefahamika baada ya zoezi la utambuzi wa miili kukamilika. Kundi la Hamas linatajwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na Ujerumani kuwa ni la kigaidi.
Qatar na Misri watoa wito wa kupunguzwa machafuko Ukanda wa Gaza
Mjini Cairo, viongozi wa Qatar na Misri wamefanya mazungumzo, huku kwa pamoja wakitoa miito ya kupunguzwa kwa machafuko katika Ukanda wa Gaza na misaada zaidi ya kiutu kuwafikia watu kwenye eneo hilo.
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi amejadiliana na kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al Thani juu ya juhudi zaidi za kuhakikisha mapigano yanasitishwa na hatua za kuongeza misaada ya kiutu kwa takriban watu milioni 2.3 waliopo Ukanda wa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya al-Sissi.
Wawili hao aidha walizungumzia kuongezeka kwa mashambulizi ya majeshi ya Israel na chhangamoto ya kikanda iliyoko mbele yao inayoupeleka ukanda huo kwenye mwelekeo wa hatari zaidi na ambao haukutarajiwa.
Saudi Arabia yatoa wito wa vita kumalizwa
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman ametoa wito wa kumalizwa vita katika Ukanda wa Gaza, huu ukiwa ni msimamo wake sambamba na azimio la viongozi wa Afrika wanaohudhuria mkutano wa kilele wa maendeleo kati ya Saudi Arabia na Afrika, huko mjini Riyadh.
Soma pia: Israel yaendeleza hujuma kwenye Ukanda wa Gaza
Bin Salman amesema kwenye mkutano huo kwamba wanalaani kile kinachotokea Gaza, na hasa mashambulizi yanayowalenga raia na ukiukwaji wa sheria ya kimataifa unaofanywa na mamlaka za Israel na kuhimiza umuhimu wa kumaliza vita hivyo, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mwanamfalme huyo kuzungumzia mzozo huo hadharani tangu ulipozuka mwezi uliopita.
Azimio la pamoja na viongozi kwenye mkutano huo wa kilele limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya kiutu huko Gaza na kutoa wito wa kumalizwa operesheni ya kijeshi na raia kulindwa.
Umoja wa Mataifa wairai Israel kufungua kivuko cha mpakani cha Kerem Shalom
Umoja wa Mataifa umeiomba Israel kufungua kivuko chake kilichoko mpakani cha Kerem Shalom ili misaada zaidi ya kiutu iweze kupita na kuingia Gaza. Kivuko hicho kilichoko kati ya Gaza na Israel kina uwezo wa kupitisha malori, tofauti na kivuko cha Rafah kinachotokea Misri, ambacho kilijengwa kwa ajili ya watembea kwa miguu.
Soma pia:Ufaransa yaandaa kongamano la kibinaadamu kwa ajili ya Gaza