Miili mitano wa waumini yafukuliwa Kenya
22 Agosti 2025Kamishina wa Kaunti ya Kilifi Josephat Biwott ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa miili ya watu hao watano imepatikana katika makaburi 4 akiongeza kuwa wamepata miili zaidi katika maeneo mengine 27.
Shughuli ya kufukua miili hiyo bado inaendelea katika eneo hilo lililoko viungani mwa mji wa Malindi, karibu na eneo la Shakahola ambako mamia ya waumini waliokuwa wanashurutishwa kufunga, walipatikana wakiwa wamefariki, miaka miwili iliyopita.
Mnamo mwezi Julai, afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ya Kenya ilisema inaamini wahanga waliozikwa katika eneo hilo, walilazimishwa kufunga kutokana na kushiriki na kuamini itikadi kali za kidini. Washukiwa 11 wanachunguzwa kuhusiana na vifo hivyo.
Zaidi ya watu 400 walikufa kwenye moja ya kisa kibaya kabisa kinachohusisha waumini wa itikadi kali za kidini kilichotambulika kama "Mauaji ya Msitu wa Shakahola" na miili yao ilifukuliwa kwenye mji wa Malindi.
Kisa hicho kiligonga vichwa vya habari sio tu kwenye taifa hilo bali pia kote ulimwenguni. Mchungaji Paul Mackenzie aliyekuwa kiongozi wa waumini hao aliowahimiza kufunga hadi kufa ili waingie mbinguni, hivi sasa anakabiliwa na kesi huko mjini Mombasa. Amekana kufanya kosa lolote la mauaji.
Maafisa walikuwa wamechimba takriban maeneo 27 kwenye ukanda huo wa pwani katika eneo la ekari tano karibu na kijiji cha Binzaro, huko Kilifi, afisa wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Robert Kiinge aliambia AFP na kuongeza kuwa wamepata miili hiyo mitano.
Kiinge alisema kuwa mabaki ya miili mingi yalikuwa yameoza kwa kiasi kikubwa, hali inayoashiria kuwa ilikuwa ardhini kwa zaidi ya mwaka mmoja, japokuwa alisema huenda mmoja alizikwa hivi karibuni kati ya miezi saba hadi minane iliyopita.
"Tulipata mabaki ya watoto wawili," alisema, akikadiria umri wao kuwa kati ya miaka mitano na saba. "Ukiangalia tunachofanyia kazi sasa hakuna shaka kuna uhusiano na mzee wa Shakahola,” alisema.
Watu 11 wametiwa mbaroni, Kiinge alisema, ingawa watatu kati yao wanachukuliwa kama waathiriwa. "Watu tulio chini ya ulinzi leo ni wafuasi wa Mackenzie," alisema.
Uchunguzi unaendelea, Kiinge aliongeza na kubainisha kuwa hadi uchunguzi wa maiti utakapopangwa hawawezi kubashiri chanzo cha vifo hivyo.