Miili iliyopatikana katika ajali ya Air India yafikia 279
14 Juni 2025Polisi wa India wamesema hii leo kwamba hadi kufikia sasa miili ya watu iliyokwishapatikana katika ajali ya ndege ya shirika la Air India imefikia 279 kutoka katika eneo la ajali.
Ongezeko hilo linaifanya ajali hiyo kuwa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya ajali za ndege katika karne ya 21. Air India ilisema ndege hiyo ilikuwa imebeba watu 242 kuelekea uwanja wa ndege wa Gatwick jijini London Uingereza, na abiria mmoja tu ndiye amenusurika.
Watu wengine 38 walipoteza maisha baada ya ndege hiyo kuanguka siku ya Alhamisi katika eneo la makazi ya raia karibu na uwanja wa ndege.
Maafisa walitangaza siku ya Ijumaa kukipata moja ya kisanduku cheusi kati ya viwili vya ndege juhudi za kutafuta kisanduku cha pili zikiendelea sambamba na zoezi la kuitafuta miili ya watu.