Miili 50 yagunduliwa kwenye makaburi ya pamoja, Libya
9 Februari 2025Mkasa huo wa Libya ni wa hivi punde unaohusisha watu wanaotaka kufika barani Ulaya kupitia kwenye nchi hiyo ya Afrika Kaskazini inayokumbwa na machafuko. Idara ya usalama imesema kaburi la kwanza lilikuwa na miili 19 katika shamba moja kusini mashariki mwa mji wa Kufra, na kwamba maiti hizo zimechukuliwa ili kufanyiwa uchunguzi kuweza kuwabaini watu hao waliokufa. Shirika la hisani la al-Abreen, ambalo huwasaidia wahamiaji mashariki na kusini mwa Libya, limesema maiti za watu wengine zinaonesha waliuawa kwa kupigwa risasi kabla ya kuzikwa kwenye kaburi la pamoja. Makundi ya kutetea haki za binadamu na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa miaka kadhaa yamekuwa yakiratibu na kuhifadhi kumbukumbu kuhusu unyanyasaji wa wahamiaji nchini Libya ikiwa ni pamoja na kazi za kulazimishwa, kupigwa, kubakwa na mateso mengine. Wahanga ni wahamiaji wanaokata kwenda Ulaya kutafuta maisha bora.