Miili 200 ya watu yapatikana mjini Mariupol
24 Mei 2022Mshauri wa meya wa mji wa Mariupol Petro Andryushchenko amesema miili hiyo imepatikana chini ya jengo moja la ghorofa lililoporomoka, na kwamba ilikuwa imeoza na inatoa harufu mbaya.
Tangazo la kupatikana kwa miili hiyo limetolewa muda mfupi tu baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy kuishtumu Urusi kwa kuendesha kile alichokiita vita kamili dhidi ya Ukraine, akilenga kufanya uharibifu mkubwa na kusababisha vifo vya watu wengi.
Soma pia: Scholz atetea uamuzi wa kuipatia Ukraine silaha
Mji wa Mariupol, ambao sasa uko chini ya udhibiti kamili wa Urusi, umeshuhudia hujuma mbaya zaidi ya vita hivyo na umekuwa kama ishara duniani kote kwa jinsi wapiganaji wa Ukraine walivyojitolea kufa kupona kuulinda.
Urusi sasa imelekeza nguzu zake zote katika kitovu cha viwanda, mashariki mwa Donbas sehemu ambayo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi na kuuzingira mji wa Sievierodonetsk na viunga vyake. Eneo hilo la Donbas Luhansk ndio sehemu pekee iliyoko chini ya udhibiti wa serikali ya Ukraine.
Biden asema mzozo wa Ukraine ni changamoto ya kimataifa
Rais wa Marekani Joe Biden ameutaja mzozo wa Ukraine kama changamoto ya kimataifa.
Katika mkutano wa kilele wa mataifa manne ya ukanda wa Indo-Pasifiki yakiwemo Japan, India na Australia, Biden amesema, "Tumejadili pia athari za uvamizi wa kikatili wa Urusi nchini Ukraine na usio na sababu, athari zake duniani kote. Marekani na India zitaendelea kushauriana kwa karibu juu ya jinsi ya kukabiliana na athari hizo."
Tofauti na Japan, Australia na Marekani, India inaonekana kuwa na msimamo wa kati juu ya vita vya Ukraine na haiungi mkono vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi.
Soma pia:Urusi: Mamia ya askari wa Ukraine wamejisalimisha
Katika mkutano huo, Biden hakuzungumzia hadharani juu ya msimamo wa India katika mzozo wa Urusi lakini mara sio moja, Marekani na washirika wake wa Magharibi wamekuwa wakifanya juhudi za mchwa kuishawishi India kujitenga na Urusi.
Tangu jadi, nchi hiyo ya kusini mwa Asia imekuwa na uhusiano mzuri na Moscow na imekuwa ikinunua silaha kutoka Urusi.
Ama kwa upande mwengine, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema haikubaliki kuwa baadhi ya mataifa duniani yanaiunga mkono Urusi katika vita vyake na Ukraine. Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi habari akiwa mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Scholz ameongeza kuwa ni muhimu kujadili juu ya madhara ya vita hivyo kama njia mojawapo ya kuhakikisha vita venyewe vinasitishwa.
Afrika Kusini ilijizuia kupiga kura katika azimio la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Machi la kulaani uvamizi wa Urusi.