Kumbukumbu ya miaka 5 tangu mauaji ya George Floyd
26 Mei 2025Kule ambako awali kulikuwepo herufi kubwa za manjano zilizosema "Black Lives Matter" (Maisha ya Weusi Ni Muhimu) katika barabara ya 16 jijini Washington, sasa kuna magari makubwa ya SUV. Maandishi hayo yaliondolewa mwezi Machi baada ya Warepublikan katika Kongresi kutishia kusitisha ufadhili wa serikali kuu kwa mji wa Washington.
Keyonna Jones, mmoja wa wasanii waliopaka maandishi hayo, aliiambia DW kwamba hilo halikupunguza uzito wa maana ya kile kilichokuja kujulikana kama "Black Lives Matter Plaza".
"Inahisi kuwa na nguvu hata ilipoondolewa,” alisema. "Ni mchanganyiko wa hisia: shukrani, kusongwa, kukatishwa tamaa, lakini pia kupewa nguvu kwa sababu sanaa ina uwezo wake.”Polisi aliyemuua George Floyd ajeruhiwa jela
Yeye pamoja na wasanii wengine walianza kupaka herufi kubwa hizo karibu miaka mitano iliyopita usiku wa manane. Kulipopambazuka, na watu wasiojulikana waliposimama kuwasaidia, walitambua kuwa walikuwa sehemu ya jambo kubwa lenye athari ya kimataifa.
Jones aliiambia DW kuwa alihisi shukrani kuwa "mmoja kati ya wasanii saba waliopaka mchoro uliorudiwa duniani kote ndani ya saa 24 tu baada ya kuupaka.” Alisema hilo lilimpa nguvu: "Ndivyo mabadiliko yanavyotokea.”
‘Siwezi kupumua'
Mabadiliko aliyotaka Jones, na bado anayatamani, ni haki na usawa. Ni miaka mitano sasa tangu George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika, auwawe katika jiji la Minneapolis, Marekani, baada ya kusimamishwa na polisi.
Afisa mzungu wa polisi alimkalia mgongoni na shingoni kwa zaidi ya dakika tisa, na kumsababisha kukosa hewa. Wakati akifa, Floyd alikuwa akirudia kusema: "Siwezi kupumua.”
Mauaji hayo yalinaswa kwenye kamera, na video hiyo ilisambaa kwa kasi. Watu waliingia mitaani kuandamana dhidi ya ukatili wa polisi na kutaka mageuzi makubwa.
Kwa mamilioni ya watu walioungana, vuguvugu la Black Lives Matter (BLM) likawa moja ya harakati kubwa zaidi za maandamano katika historia ya Marekani.
Jinsi vuguvugu la BLM lilivyoenea duniani
Lakini BLM halikusalia Marekani pekee. Kulikuwa na maandamano duniani kote kwa mshikamano na George Floyd, waandamanaji wakianza kuuliza maswali kuhusu serikali zao wenyewe. Nchini Brazil na Colombia, waandamanaji walipinga ukatili wa polisi wa kibaguzi dhidi ya watu wa jamii ya Wenyeji na Weusi.
Barani Ulaya, maelfu ya watu walijitokeza mitaani. Maandamano makubwa yalifanyika Denmark, Italia, na Ujerumani. Tahir Della, msemaji wa kundi la Initiative Black People in Germany, aliiambia DW kwamba maandamano hayo yalionyesha "kuna uelewa unaokua kuhusu tatizo hili."
"Mauaji ya George Floyd yanaweza kuchukuliwa kama hatua ya mabadiliko,” alisema wakili Laila Abdul-Rahman, mtafiti wa ukatili wa polisi katika Chuo Kikuu cha Goethe, Frankfurt. Alisema BLM lilichangia sana katika kuleta mjadala mpya nchini Ujerumani pia. "Mazungumzo yamebadilika, hata katika vyuo vikuu.”
‘Jina lake ni George Floyd'
Hata hivyo, miaka mitano baada ya mauaji ya George Floyd, kuna hali ya kukatishwa tamaa. Matumaini ya awali kuwa maandamano yangeleta mabadiliko hayakutimia, hasa nchini Marekani. "Hatujaona mabadiliko yote ambayo watu waliahidiwa,” alisema Robert Samuels, mwandishi mwenza wa kitabu kilichoshinda tuzo ya Pulitzer His Name is George Floyd, pamoja na Toluse Olorunnipa.
"Na ambacho hakijabadilika ni kwamba taifa hili bado halijaweka juhudi endelevu kuhakikisha usawa na fursa kwa wote,” Samuels aliiambia DW.
Wakati mwaka 2020, asilimia 52 ya Wamarekani waliamini kuwa maisha ya Weusi yangeboreshwa, kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha Pew Research Center, sasa ni asilimia 27 tu wanaoamini maandamano yalileta mabadiliko chanya, huku asilimia 72 wakiona hakuna kilichobadilika.
Trump abatilisha mipango ya DEI
Hali hii inaweza kuwa na uhusiano na Rais Donald Trump: Muda mfupi baada ya kuingia tena madarakani mwaka huu, aliamuru mipango yote ya kukuza utofauti, usawa, na ujumuishaji (DEI) katika mashirika ya serikali kusitishwa.
Maagizo ya kiutendaji yaliyohimiza kampuni na vyuo vikuu kukuza fursa sawa na kuzuia ubaguzi dhidi ya makundi yaliyotengwa yalifutwa.
Utawala wa Trump pia ulitishia kuondoa ufadhili wa serikali kwa shule za umma kama njia ya kuwalazimisha kuondoa programu za utofauti na kufundisha kuhusu ubaguzi wa rangi na haki za kijamii.
Serikali ya Marekani pia imetangaza kuwa itasitisha kesi kadhaa dhidi ya idara za polisi katika majimbo mbalimbali, na hivyo kusitisha uchunguzi ulioanzishwa baada ya mauaji ya George Floyd. Wizara ya Sheria ilisema mbinu iliyotumika kuchunguza tuhuma za ubaguzi wa kimfumo ilikuwa na dosari.
Kulingana na mradi wa Mapping Police Violence, polisi waliwaua angalau watu 1,260 nchini Marekani mwaka 2024 — idadi kubwa zaidi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Mradi huo unasema Wamarekani Weusi wana uwezekano mara 2.8 zaidi kuuawa na polisi ikilinganishwa na Wazungu. Keyonna Jones aliiambia DW kwamba amepoteza marafiki wake sita waliouawa na polisi au kupigwa risasi katika mtaa wake.
Ni vigumu kujua kwa uhakika ni watu wangapi duniani wamekuwa waathirika wa ukatili wa polisi wa kibaguzi, na iwapo idadi hiyo imebadilika. Mashirika ya haki za binadamu yanasema katika nchi nyingi, vifo hivyo haviripotiwi.
Mwaka 2024, shirika la Amnesty International liliandika kuwa nchini Brazil, polisi waliwaua mara kwa mara watu wasiokuwa na tishio, hasa vijana Weusi, wakijua kwamba mauaji hayo hayatapelelezwa wala kufikishwa mahakamani.
‘Watu Weusi wamejifunza kuishi'
Hata hivyo, Samuels anasema kuna alau mabadiliko chanya nchini Marekani, hasa katika jinsi watu wanavyozungumza kuhusu ubaguzi wa rangi.
Anasema pia kwamba angalau majimbo 16 yamepiga marufuku mbinu ya polisi ya kuwawekea magoti shingoni washukiwa — mbinu iliyosababisha kifo cha Floyd.
Kuhusu utawala wa sasa, Jones anasema kwa mtazamo wa kukubaliana na hali: "Trump si jambo la msingi kwangu. Watu Weusi tumeshajifunza jinsi ya kuishi tangu enzi, vizazi hadi vizazi.
Nikiwa mzaliwa na mkazi wa D.C., hasa Kusini Mashariki mwa D.C., ambako tuna upungufu wa huduma au tunasahaulika, simulizi ya maisha ya kujinusuru si jambo jipya kwangu. Kwa hiyo hata mtu mpya akiingia madarakani, hainishtui kabisa.”