Miaka 10 ya kauli ya Merkel ‘Tutaweza!’
31 Agosti 2025Jumapili hii inatimiza miaka kumi tangu Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel kutoa kauli yake maarufu "Wir schaffen das” — "Tutaweza” — wakati taifa hilo lilipofungua mipaka kwa wimbi kubwa la wakimbizi waliokimbia vita nchini Syria, Afghanistan na Iraq.
Wakati huo, kauli hiyo ilionekana kama ishara ya matumaini na uthibitisho wa mwelekeo mpya wa Ujerumani, ikionesha kuwa taifa lililokuwa limegawanyika wakati wa Vita Baridi na lililokuwa na historia ya Holocaust sasa lipo tayari kuonyesha mshikamano wa kibinadamu.
Hata hivyo, miaka kumi baadaye, mjadala kuhusu uhamiaji umegeuka na kuwa miongoni mwa masuala yanayogawanya zaidi taifa hilo, huku mafanikio, changamoto na athari zake zikijitokeza kwa uwazi zaidi.
Kati ya mwaka 2015 na 2016 pekee, zaidi ya watu milioni 1.2 waliomba hifadhi nchini Ujerumani, na kufanya taifa hilo kuwa nchi ya Umoja wa Ulaya iliyoongoza kwa idadi ya wakimbizi waliopokelewa.
Leo hii, takriban watu milioni 3.5 wanaoomba hifadhi au waliopata hadhi ya ulinzi wanaishi Ujerumani, wengi wao wakiwa ni Wasyria, Waafghani, Wairaqi na Waukraine waliokimbia uvamizi wa Urusi mwaka 2022.
Kwa mfano, nusu ya Wasyria walioko Ujerumani waliwasili kati ya 2014 na 2016, huku takriban moja ya tano wakiwa tayari wamepewa uraia, na wengine wakizingatia kusalia kutokana na uwekezaji na familia walizojenga nchini humo.
Mchanganyiko wa mafanikio na changamoto
Katika suala la ujumuishaji, takwimu zinaonyesha mchanganyiko wa mafanikio na changamoto. Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Ajira (IAB), kufikia mwaka 2022 karibu asilimia 66 ya wakimbizi waliowasili mwaka 2015 walikuwa wamepata ajira.
Hata hivyo, ukosefu wa ajira miongoni mwa wahamiaji bado ni wa juu mno, ukiwa asilimia 28 mwaka 2024 — mara nne ya wastani wa kitaifa. Aidha, tofauti za kijinsia pia zinaonekana wazi.
Utafiti wa mwaka 2020 unaonyesha kwamba asilimia 54 ya wanaume walifikia kiwango cha kati cha lugha ya Kijerumani (B1), ilhali wanawake walikuwa asilimia 34 pekee, jambo linaloathiri nafasi zao katika soko la ajira.
Zaidi ya watu 414,000 kutoka nchi zinazochukuliwa kuwa vyanzo vikuu vya wakimbizi, wakiwemo zaidi ya 240,000 wa Syria, wamepata uraia wa Ujerumani tangu 2016. Watafiti wanasema wengi wao sasa wamesalia kwa sababu ya ajira, elimu ya watoto wao na biashara walizoanzisha.
Hata hivyo, mabadiliko ya sera pia yamekuwa makubwa. Tangu 2015, sheria za hifadhi zimewekewa masharti makali zaidi, misaada ya kifedha kwa waomba hifadhi imepunguzwa, na urejeshaji wa wahamiaji wasio na vibali umeongezeka.
Merz asema utekelezaji wa "Tutaweza" haujafulu
Chini ya Kansela wa sasa Friedrich Merz, ambaye anatoka chama kile kile cha CDU cha Merkel, serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kudhibiti mipaka, kupunguza idadi ya wanaoomba hifadhi na kuongeza idadi ya wanaorudishwa makwao.
Merz ameenda mbali na kusema kuwa Ujerumani "haijafaulu” kutekeleza kauli ya "Tutaweza,” akisisitiza kuwa sasa ni lazima kudhibiti uhamiaji na kuhakikisha ujumuishaji bora zaidi kwa wale wanaokubaliwa kubaki.
Zaidi ya changamoto za kiuchumi na ajira, mjadala wa uhamiaji umegeuka kuwa suala lenye hisia kali kisiasa na kijamii.
Chama cha mrengo wa kulia kinachopinga uhamiaji, Alternative für Deutschland (AfD), kimepata umaarufu mkubwa na sasa kimekuwa chama cha pili kwa ukubwa bungeni, kikitumia hofu za usalama na changamoto za kijamii kujijengea mtaji wa kisiasa.
Ripoti za polisi zinaonyesha kuwa wageni wanatajwa katika asilimia 35 ya kesi za uhalifu, ingawa ni asilimia 15 pekee ya wakaazi wote, hali ambayo wachambuzi wanasema inatokana zaidi na uonevu wa takwimu kuliko ukweli wa moja kwa moja kuhusu uhalifu miongoni mwa wakimbizi.
Gharama za kifedha pia zimekuwa kubwa. Mwaka 2023 pekee, Ujerumani ilitumia euro bilioni 30 kwa ajili ya huduma za kijamii, elimu, mafunzo ya lugha na misaada mingine kwa wakimbizi.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema muda mrefu unaweza kuonyesha faida, kwani wengi wa wahamiaji sasa wanalipa kodi na kuchangia katika soko la ajira, haswa kutokana na uhaba wa nguvu kazi unaolikabili taifa hilo linalozeeka kwa kasi.
Mabadiliko ya hisia za umma
Lakini pengine mabadiliko makubwa zaidi yako katika hisia za umma. Mwaka 2015, Wajerumani wengi walipokea wakimbizi kwa moyo mkunjufu, wakiunganishwa na wimbi la mshikamano wa kijamii.
Hata hivyo, mwaka 2024, tafiti zinaonyesha asilimia 68 ya wananchi wanasema Ujerumani inapaswa kupunguza idadi ya wakimbizi. Sababu kuu zinazotolewa ni hofu ya mzigo kwa mfumo wa ustawi wa jamii na migongano ya kitamaduni, huku wachambuzi wakionya kuwa mijadala hii imeongeza mgawanyiko wa kisiasa na kuimarisha vyama vya mrengo mkali wa kulia.
Licha ya mabadiliko haya yote, watafiti kama Profesa Hannes Schammann wa Chuo Kikuu cha Hildesheim wanasema Ujerumani kwa kiwango kikubwa imefanikiwa kukabiliana na changamoto za mwaka 2015.
Anasema mjadala sasa unapaswa kuangalia mbele badala ya kushikilia yaliyopita, akisisitiza haja ya kuunda sera bora za muda mrefu zinazoweza kusawazisha utu, usalama na maslahi ya kiuchumi ya taifa.
Miaka kumi baada ya kauli ya "Tutaweza,” Ujerumani inajikuta kwenye makutano ya kihistoria: taifa linalojivunia ukarimu wake lakini pia linakabiliwa na shinikizo la kisiasa, changamoto za ujumuishaji na mgawanyiko wa kijamii.
Swali kubwa linalosalia ni jinsi litakavyosawazisha maslahi haya yanayokinzana huku likibaki na sera thabiti za uhamiaji kwa vizazi vijavyo.